Watumishi wa sekta ya Afya wametakiwa kuacha tabia ya kutoka kazini muda wa kazi na kwenda kufanya kazi zao binafsi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel baada ya kufanya kikao kazi na mameneja wa Mikoa toka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya nchini NHIF Jijini Dodoma.

“Waziri wa Afya aliunda timu na ikaonyesha jinsi ambavyo kuna ubadhirifu mkubwa kwenye eneo la dawa, kuna madaktari hawakai wakati wa kazi, dawa zinaibiwa na kukosesha huduma kwa wananchi na kuikosesha Serikali mapato” amesema Dkt. Mollel.

Dkt. Mollel ameonyesha kushangazwa na viongozi ndani ya maeneo husika kushindwa kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi wenye tabia hizo huku akisisitiza watumishi wenye tabia hizo kujirekebisha kabla ya yeye kuanza kuchukua hatua za kisheria.

“Kila mtu acheze kwenye namba yake sasa, usipocheza kwenye namba yako imekula kwako, usifikiri usipocheza kwenye namba yako itamhusu yule aliyefanya kosa, itakuhusu na wewe ambaye ulitakiwa uone” amesema Dkt. Mollel

Ametoa onyo pia kwa wamiliki wa vituo binafsi vya kutolea huduma za afya nchini kuhakikisha wanafuata taratibu zote walizopewa kwenye usajili wa vituo hivyo na kuacha kutumia watumishi wa umma kinyume na taratibu za muda wa kazi.

Huu hapa uwanja wa Geita Gold FC
Idadi ya mashabiki viwanjani itaongeza maambukizo ya corona