Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Norway hapa nchini Bi. Hanne-Marie Kaarstad na kutoa wito kwa wawekezaji kutoka Norway kuja kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo Nishati, misitu, kilimo, gesi na mafuta.
Ametoa mwaliko huo leo jijini Dar es salaam mara baada ya kukutana na balozi huyo, ambapo amesemweleza kuwa Tanzania iko katika hatua mbalimbali za kukuza uchumi wake kupitia sekta ya viwanda na kwamba wawekezaji kutoka Norway watakuwa na mchango mkubwa wa kuiwezesha Tanzania kufikia lengo hilo.
“Tumeamua kujenga Reli ya Kati kwa viwango vya kimataifa-SGR ambayo inahitaji umeme wa kutosha kwa hiyo bado tunahitaji mchango wa wadau mbalimbali ikiwemo Norway ili kuhakikisha kuwa tunakuwa na nishati ya umeme ya kutosha na ya uhakika ili kufanikisha mradi huo mkubwa,” amesema Dkt. Mpango
Aidha, kuhusu Sekta Binafsi, Dkt. Mpango amesema kuwa Serikali imeendelea na majadiliano na Sekta hiyo ili kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili ikiwemo masuala ya kodi pamoja na kujenga kuaminiana kati ya pande hizo mbili.
Kwa upande wake Balozi wa Norway hapa nchini Bi. Hanne-Marie Kaarstad amesema kuwa nchi yake imeridhika na namna Serikali ya Awamu ya Tano inavyopiga hatua kubwa katika maendeleo ya watu wake kupitia kuhamasisha uchumi wa viwanda.
-
Benki za Wananchi zawekwa mtegoni
-
Manyanya awataka wataalam kubadilishana uzoefu
-
JPM amwaga bilioni 210 za mradi
Amesema kuwa nchi yake imesaini mikataba mikubwa miwili hivi karibuni ukiwemo mkataba wa msaada wa krona milioni 600 (fedha za Norway) kwa ajili ya mradi wa kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini-REA, hatua anayoamini kuwa itaharakisha maendeleo na uchumi wa kati wa nchi ifikapo mwaka 2025 na kuongeza kuwa nchi yake itaendeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili.