Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amelielekeza Baraza la ushauri la watumiaji wa huduma za mawasiliano (TCRA- CCC) kufanya tathmini ya malalamiko yanayotolewa na wananchi dhidi ya kampuni za simu kuhusu kukatwa na kuibiwa vifurushi ambapo ameagiza swala hili kupatiwa ufumbuzi.
Dkt. Ndugulile ametoa maelekezo hayo alipokutana na watendaji wa baraza hilo pamoja na Tume ya Taifa ya Tehama, amabpo amesema waangalie utendaji wa taasisi hizo za simu na namna zinavyoweza kusaidia Serikali kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia.
Hata hivyo, Ndungulile amesema kuwa kumekuwa na malalamiko mengi ya wananchi kuhusu vifurushi vinavyotolewa na kampuni za simu hivyo ni muhimu kuyafanyia kazi ili ufumbuzi wake upatikane.
Amesema taarifa alizonazo ni kwamba wananchi wanalalamikia huduma za vifurushi ikiwemo kupunjwa na kutozwa fedha nyingi tofauti na data au muda wa maongezi wanaopewa na kutaka suala hilo kupatiwa ufumbuzi.
Aidha ametoa rai kwa wananchi kuitumia vizuri mitandao kwa kuwa sheria zipo na hataki ifike wakati serikali inaingia kwenye mikinzano na wananchi kwa sababu ya mitandao.