Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wamepongezwa kutokana na jitihada kubwa za kukuza diplomasia ya uchumi zilizofanyika mwaka 2022.
Pongezi hizo zimetolewa jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax wakati wa kikao chake cha kwanza na watumishi wa Wizara tangu kuteuliwa kushika wadhifa huo Oktoba 2022.
Ameyataja maeneo ambayo Wizara imeyaratibu kwa ufanisi unaoridhisha kuwa ni pamoja na ziara za viongozi wa kitaifa nje ya nchi, ushiriki wa viongozi katika mikutano ya kikanda na kimataifa, na uandaaji wa mikutano ya Tume za Kudumu za Pamoja za Ushirikiano (JPCs).
Amesema majukumu hayo ambayo sio mepesi kuyatekeleza, yamekuwa na manufaa makubwa nchini katika nyanja za kidiplomasia na uchumi na kuwasihi watumishi kuendeleza jitihada hizo kwa kuzingatia weledi, uzalendo na uadilifu katika kusimamia maslahi ya Taifa.