Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax ameongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa 42 wa Baraza la Mawaziri la Umoja wa Afrika unaofanyika Addis Ababa tarehe 15 – 16 Februari 2023.
Akichangia katika mkutano huo, Dkt. Tax alisisitiza umuhimu wa Kamisheni na Taasisi za Umoja wa Afrika kusimamia vyema rasilimali za Umoja wa Afrika kwa kuchukua hatua za kuondoa mapungufu yaliyobainika kwenye taarifa ya ukaguzi wa rasilimali za Umoja wa Afrika.
Mkutano wa Mawaziri utajadili masuala ya kimkakati yanayohusu Bara la Afrika ikiwemo utekelezaji wa Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika-AfCFTA, uhakika wa chakula, hali ya ulinzi na usalama, mabadiliko ya tabianchi, pamoja na masuala ya kiutawala na usimamizi wa rasilimali za Umoja wa Afrika.
Aidha, Waziri pia alieleza hatua ambazo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inachukua katika kutekeleza Mikataba ya Uenyeji ya Taasisi za Umoja wa Afrika zilizopo Tanzania ambazo ni Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Umoja wa Posta Afrika na Bodi ya Umoja wa Afrika ya Ushauri dhidi ya Rushwa.
Awali, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Moussa Faki Mahamat alisisitiza umuhimu wa Umoja wa Afrika kuendelea kutoa kipaumbele kwenye masuala yanayowagusa wananchi wa Afrika ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto mbalimbali za mabadiliko za kijamii, kiuchumi na kiusalama.
Mkutano huu ni sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika utakaofanyika tarehe 18-19 Februari 2023.