Rais wa Umoja Wa Mabunge Duniani – IPU, Dkt. Tulia Ackson ameielekeza kamati inayoshughulikia masuala ya Mashariki ya Kati ya Umoja huo kutembelea eneo hilo mapema katika juhudi za kutafuta suluhisho linaloweza kuhakikisha amani na usalama vinapatikana kufuatia mgogo unaoendelea baina ya Israel na Palestina.
Dkt. Tulia ameysema hayo Jijini Tel Aviv nchini Israel mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku mbili iliyompa fursa ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Israel na Mamlaka ya Palestina.
“Nimekuja kutembelea maeneo ya Palestina na Israel ambao wote hawa mabunge yao ni wanachama wa IPU lakini muhimu zaidi ni kuwafahamsha kuwa tupo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu na kamati yetu inayoshughulikia masuala ya Mashariki ya Kati itakuwa hapa siku zijazo kutatafuta uhalisia wa mgogoro huu na kuleta taarifa ambayo tutapata nafasi ya kuijadili ili tuone huko mbele tunakokwenda tunawezaje kuwa na amani na usala kwa watu wote” amesema Dkt.Tulia
Aidha, amesema Mpango mkakati wa umoja huo ni kuutumia mwaka 2024 pamoja na mambo mengine kujadili kwa kina suala la amani na usalama kama ajenda muhimukwenye mikutano yake mikuu ya mwezi machi na oktoba mwakani.
Dkt. Tulia na Ujumbe wake amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa mamlaka ya Palestina jijini Ramallah akiwemo Wazri Mkuu wa Mamlaka hiyo, Muhammad Shtayyeh pamoja na Spika wa Baraza la Mamlaka yaPalestina, Rawhi Fattouh.
Hata hivyo, Dkt.Tulia alipata fursa ya kutembelea kijiji cha Kfar Kibbutz kati ya vijiji vilivyoshambuliwa na wanamgambo wa Hamas Oktoba 7, 2023 na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Israel (Knesset) Amir Ohana, Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya vijij, Avi Dicter na wabunge wawakilishi wa Knesset kweye IPU waliongozwa na Danny Daddon.