Afisa habari wa klabu ya Dodoma jiji Moses Mpunga amelalamika kuwa chumba cha wachezaji wao ndani ya Uwanja wa Mkapa kimepuliziwa Dawa.
Mpunga ametoa madai hayo kabla ya kuanza kwa mchezo wa nne wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ kati ya timu yake Dodoma Jiji FC dhidi ya mabingwa watetezi wa michuano hiyo Simba SC.
Amesema viongozi walioambatana na timu kwenye safari ya Dar es salaam na benchi la ufundi wamejiridhisha kuwepo kwa hewa nzito katika chumba cha kubadilishia.
Amesema kutokana na hali hiyo wachezaji walitakiwa kupumzika kwenye chumba kingine uwanjani hapo, ili kuepuka madhara ambayo huenda yangewaathiri kabla na wakati wa mchezo wao dhidi ya Simba SC.
“Chumba chetu cha kubadilishia nguo hapa katika uwanja wa Mkapa kimepuliziwa dawa, kuna harufu kali sana ya dawa hivyo tumemwagia maji ili kuikata na wachezaji tumewatafutia chumba kingine cha kupumzika kwa muda” amesema Moses Mpunga Afisa Habari Dodoma Jiji.
Tayari timu za Young Africans, Biashara United Mara na Azam FC zimeshatinga Nusu Fainali ya michuano hiyo ya ASFC.
Young Africans ilifuzu kucheza hagua hiyo baada ya kuifunga Mwadui FC mabao mawili kwa sifuri jana Jumanne mkoani Shinyanga, huku Biashara United Mara wakiivurumusha Namingo FC kwa mabao mawili kwa sifuri.
Azam FC leo jioni iliifunga Rhino Rangers ya Tabora mabao matatu kwa moja.
Young Africans watacheza nusu fainali dhidi ya Biashara United Mara mwezi ujao, huku Azam FC ikimsubiri mshindi kati ya Simba SC dhidi ya Dodoma Jiji FC.
Ikumbukwe kuwa bingwa wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ‘CAFCC’ msimu ujao 2021/22.
Bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara atapata fursa ya kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ‘CAFCL’ msimu ujao 2021/22.