Mshambuliaji wa pembeni wa mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC Douglas Costa, amefungiwa kucheza michezo minne, kufuatia kosa la kumtemea mate kiungo wa klabu ya Sassuolo Federico Di Francesco, wakati wa mchezo wa ligi uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita mjini Turin.

Costa alitolewa nje kwa kadi nyekundu kufuatia kosa hilo, lakini kabla ya hapo aliepuka adhabu kama hiyo, baada ya kumpiga kiwiko Di Francesco, ambaye alionyesha kummudu mshambuliaji huyo kutoka nchini Brazil kabla ya hajaadhibiwa na mwamuzi.

Katika mchezo huo Juventus walichomoza na ushindi wa mabao mawili kwa moja, licha ya kuwa pungufu.

Tayari Costa ameshawaomba radhi mashabiki pamoja na wachezaji wenzake wa Juventus kwa utovu wa nidhamu alioufanya.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28, atakosa michezo ya ligi ya Italia dhidi ya Frosinone, Bologna, Napoli na Udinese, lakini kwa upande wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya ataonekana kama kawaida.

Leo usiku Juventus wataikabili Valencia ya Hispania katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza wa kundi H.

 

Video: Lissu tumepigwa, CCM yamshangaa RC Makonda
Je, kinywaji cha Coca-Cola chenye bangi kitalewesha?