Watu wawili wamefariki baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na maji katika mto Gwaseni uliopo eneo la Bamba, huku Idara ya kukabiliana na majanga Kaunti ya Kilifi Nchini Kenya, ikisema watu wengine wawili waliokuwemo ndani ya gari hilo hawajulikani walipo.
Juhudi za kuitafuta miili hiyo zinaendelea huku tahadhari ikizidi kutolewa kutokana na Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha huku familia nyingi zikidaiwa kuzidi kuhama makwao huku zikipata hasara ya mali hasa katika eneo la Pwani.
Inaarifiwa kuwa Vijiji vya Mbogolo, Kakuani na Kisiwani vilivyoko wadi ya Kakuyuni na kijiji cha Nuru kilichoko Garashi eneo bunge la Magarini vnavyo vimezingirwa na maji katika kaunti ya Kilifi, kutokana na mvua ya El Nino.
Hata hivyo, Serikali imesema kaunti 38 ziko hatarini kutokana na athari za El Nino ambapo Msemaji wa Ikulu, Hussein Mohamed amesema Baraza la Mawaziri limeafiki kukusanya shilingi billion 7 kukabiliana na hali hiyo huku takwimu zikionyesha watu 76 wamefariki na zaidi ya elfu 35 wameyahama makazi yao.