Uongozi wa klabu ya Everton umeendelea kufanya utaratibu wa kuzungumza na baadhi ya mameneja ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kumsaka mrithi wa Roberto Martinez aliyeondoka mwishoni mwa msimu wa 2015-16.

Everton wameanza mchakato huo, huku jina la meneja wa mabingwa wa Europa League, Sevilla CF Unai Emery likiendelea kusalia kwenye orodha ya wanaopewa kipaumbele cha kuchukua ajira huko Goodson Park.

Meneja huyo mwenye umri wa miaka 44, tayari ameshaweka hadharani mkakati wake kuelekea msimu mpya wa ligi, kwa kuwaeleza viongozi wa klabu ya Sevilla CF kwamba, anahitaji kupata changamoto mpya baada ya kushinda taji la Europa league mara tatu mfululizo.

Hata hivyo imeripotiwa kwamba, kuna mvutano unaendelea baina ya viongozi wa Everton kuhusu mchakato wa kumpata meneja atakaekiongoza kikosi chao msimu ujao wa ligi, kutokana na baadhi yao kujigawa na kutilia mkazo kwenye majina ya watu wengine.

Muwekezaji mwenye hisa nyingi klabuni hapo Farhad Moshiri, ameonyesha kumuamini sana meneja wa sasa wa klabu ya Southampton Ronald Koeman, na amekua akisisitiza mtu huyo kupewa ajira.

Neye mwenyekiti wa Everon Bill Kenwright, amekua na mtazamo tofauti kwa kuwasilisha jina la aliyekua meneja wa klabu ya Ajax ya nchini Uholanzi Frank de Boer, Manuel Pellegrini (aliyeondoka Manchester City) pamoja na aliyekua mkuu wa benchi la ufundi klabuni hapo David Moyes ambaye kwa sasa hana kazi.

Mvutano wa kuwasilishwa kwa majina hayo, umepewa muda na kabla ya kikosi kwenda katika ziara ya kujiandaa na msimu wa 2016-17, uongozi wa Everton kwa pamoja umetakiwa kufikia makubaliano ya kutoka na jina moja la meneja ambaye atakabidhiwa jukumu la kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Ilkay Gundogan Ajiunga Rasmi Na Man City
Hugo Lloris Agoma Kusaini Mkataba Mpya