Aliekua meneja wa kikosi cha Man Utd Louis van Gaal ametangaza msimamo wa kutoendelea na shughuli za ukufunzi wa soka, kwa kigezo cha kuheshimu maamuzi ya familia yake.

Van Gaal mwenye umri wa miaka 65, ameliambia gazeti la De Telegraaf la nchini kwao Uholanzi kuwa, hana mpango wa kurejea kufundisha soka kwa kipindi hiki kutokana na ushauri aliopewa na wanafamilia.

Amesema anatamani kuwa sehemu ya mchezo wa soka, kutokana na kuufahamu na kuupenda mchezo huo, lakini bado ushauri na maamuzi ya familia yake ataendelea kuyaheshimu.

Van Gaal ameweka wazi mpango huo, kufuatia ofa iliyoipokea kutoka mashariki ya mbali (China) ambapo moja ya klabu za soka nchini humo, zimeonyesha nia ya kutaka kufanya nae kazi kwa malipo ya mshahara wa Pauni milioni 44 kwa misimu mitatu.

“Ninaweza kwenda huko, lakini bado nipo hapa,” Alisema Van Gaal. “Hakuna kingine zaidi ya kuheshimu maamuzi ya familia yangu.”

Meneja huyo ambaye aliwahi kuvinoa vikosi vya klabu za Ajax, FC Barcelona, FC Bayern Munich pamoja na timu ya taifa ya Uholanzi, aliwahi kuonyesha nia ya kutaka kuendelea na kazi ya ukufunzi mara baada ya kuondoka Old Trafford mwishoni mwa msimu uliopita.

Taarifa ambazo zimeelezwa na gazeti la De Telegraaf zinasema kuwa, ushawishi wa mzee huyo kuachana na soka kutoka ndani ya familia yake, umekuja baada ya mtoto wake wa kike kufiwa na mumewe, na jambo hilo lilitoa uzito kwa wanafamilia kumshauri ili akae pamoja na familia yake kwa kipindi hiki.

Video: Lowasa akamatwa, Majaliwa amaliza 'utata' baa la njaa...
Silaha zakamatwa pori la vikindu