Kutokana na malalamiko ya Wananchi juu ya viwango vya fidia na mkanganyiko juu ya zoezi la uthamini wa makazi, ili kupisha Mradi wa Uendelezaji wa Bonde la Mto Msimbazi, Serikali imesema uthamani haukuhusisha ardhi isipokuwa mali zisizohamishika.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Miradi ya Serikali inayofadhiliwa na Benki ya Dunia Mhandisi, Humphrey Kanyenye wakati akizungumza na Vyombo vya Habari na kuongeza kuwa, viwango vya fidia vimetokana na uhalisia wa mali zisizohamishika zilizokutwa wakati wa uthamini.
Amesema, “Kilichofanyiwa uthamini ni kile kilichokutwa kwenye eneo husika, wengi walikuwa na matarajio makubwa lakini hatukuhusisha ardhi tumeangalia kile tulichokikuta kwenye eneo husika.”
Amesema, uthamini huo haukuhusisha ardhi kwa sababu eneo hilo lilishatolewa notisi na Serikali mwaka 1979 kwamba halipaswi kuendelezwa na yeyote huku baadhi ya Wananchi wakipinga hatua hiyo na kusema Serikali haitendi haki.
“Kama tungeshikamana nina hakika tungefanikiwa kupata haki yetu. Rais hana shida ila watendaji wake maana unakuta mtu mule ndani ukilalamika sana wanaichana karatasi yako halafu wanakuongezea kiasi cha pesa sasa hapo we unaelewaje,?” aliuliza mmoja wa waathiriwa.
Hata hivyo, Wananchi hao wamesema wanamuomba Rais Samia kuingilia kati suala hilo kwani wanahisi watendaji wanaomuwakilisha wanamuangusha na kwamba kuna utaratibu unaopelekwa kinyume na kusababisha athari kwa walio wengi.