Serikali nchini, imesitisha utoaji vibali vya ukarabati kwa majengo chakavu ya chini mkoani Mwanza ili kutoa fursa ya uendelezaji upya viwanja hivyo kwa mujibu wa mpango kabambe.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula, katika kikao cha utekelezaji wa programu ya urasmishaji makazi na shughuli nyingine za sekta ya ardhi kilichofanyika jijini Mwanza.

Dkt Mabula amewataka wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo kuhakikisha ifikapo juni 2023 wanawasilisha taarifa za utekelezaji wa sheria ya mipango miji ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa mpango kabambe  na mipangokina kama ilivyoelekezwa na sheria ya mipango miji sura 355 kifungu cha 22(1).

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula.

Mipango kabambe inatoa mwongozo wa ukuaji miji na kutenga maeneo kwa ajili ya matumizi mbakimbali  na kudhibiti uendelezaji holela.

Amesema, jiji la Mwanza ni miongoni mwa majiji yanayokuwa kwa kasi hapa nchini na lenye sifa ya kuwa kitovu cha kiuchumi na kibiashara katika ukanda wa nchi za maziwa makuu na Afrika Mashariki.

Mabula amesema, serikali imefanya uwekezaji mkubwa uliogharimu kiasi cha dola za marekani 5,507, 145 sawa na shilingi 9,204,645,495.8 kwa kiwango cha dola kwa shilingi 1671.4 cha wakati huo kwa ajili ya kuandaa mpango kabambe (2015-2035) wa jiji la Mwanza.

‘’Sheria ya Mipangomiji sura 355 kupitia fungu la 7 (u) inaipa mamlaka ya jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela kusimamia na kutathmini utekekezaji wa mpango kabambe na mipangokina,’’ alisema Dkt. Mabula.

Ajali: Gari lagonga Treni Tabora
Walioathirika na mimba za utotoni wasitengwe