Gavana wa zamani wa Rwanda, Laurent Bucyibaruta, amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kuhusika na mauaji ya halaiki.
Hukumu hiyo, imetolewa ikiwa ni zaidi ya miaka 28 baada ya mauaji ya halaiki ya Watutsi mwaka 1994 wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Gikongoro uliopo magharibi mwa Rwanda.
Baada ya takriban saa kumi na moja za mashauri katika Mahakama ya Assize ya jijini Paris, mzee huyo wa miaka 78 aliachiliwa kama mhusika wa mauaji ya halaiki, lakini akapatikana na hatia ya ushiriki wa mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinadamu kwa mauaji manne.
Bucyibaruta, ambaye kesi yake ilianza Mei 9, 2022 alikuwa ni afisa wa ngazi ya juu wa Rwanda, aliyewahi kuhukumiwa nchini Ufaransa kwa uhalifu unaohusiana na mauaji ya kimbari ya Watutsi.
Gavana huyo wa zamani amekanusha kuhusika kwake na mauaji ya halaiki na amekuwa nchini Ufaransa tangu mwaka 1997 chini ya uangalizi wa mahakama ambapo sasa atakuwa mfungwa rasmi.
Hata hivyo, Bucyibaruta ana siku kumi za kukata rufaa dhidi ya hukumu yake na Mawakili wanaomtetea wamekataa kutoa maoni juu ya hukumu hiyo.
Afisa huyo mwandamizi wa zamani wa Rwanda Laurent Bucyibaruta alifikishwa mahakamani mjini Paris, akituhumiwa kuhusika na mauaji ya halaiki ya watu kwenye taifa, mwaka 1994.
Kesi yake imedumu kwa kwa miezi miwili na kushirikisha mashahidi zaidi ya 100, wakiwemo walionusurika na mkauaji hayo kutoka Rwanda ambao walisafirishwa kwa ndege na wengine walihudhuria kwa njia ya video.
Kesi ya Bucyibaruta ni ya nne kwa mauaji ya kimbari ya Rwanda kufikishwa mahakamani nchini Ufaransa, ambayo kwa muda mrefu imekuwa chini ya shinikizo kutoka kwa wanaharakati waliochukua hatua dhidi ya washukiwa wa uhalifu ambao walikuwa wamekimbilia katika ardhi ya Ufaransa.
Takriban Watutsi 800,000 na Wahutu wenye msimamo wa wastani waliuawa katika siku 100 za mauaji mwaka 1994, ambapo wanamgambo wa Kihutu waliwaua Watutsi waliokuwa wakijificha makanisani na shuleni.