Serikali imesitisha uchapishaji na usambazaji wa gazeti la kila wiki la RAIA MWEMA kwa muda wa siku 90 (miezi mitatu) kuanzia leo.

Agizo hili pia linahusu toleo la mtandaoni. Adhabu hii inatokana na toleo na. 529 la tarehe 27 Septemba–3 Oktoba, 2017 lililochapisha habari ya uchambuzi inayosomeka “URAIS UTAMSHINDA JOHN MAGUFULI.”

Serikali inasisitiza uchambuzi huu ni maoni yao ya haki (fair comment), hata hivyo, kwa bahati mbaya, na nia ovu, makala hiyo ilisheheni nukuu za kutunga na zisizo za kweli zikimsingizia Rais John Pombe Magufuli. Gazeti hili pia limepata kuonywa huko nyuma kwa makosa mbalimbali.

Nukuu za uongo, kutungwa na zenye nia mbaya zikidai Rais alipata kusema: “Suruali za zamani msizitupe, mtazihitaji baadae,” na “Watakaobaki  Dar es Salaam baada ya mwezi wa saba watakuwa wanaume kwelikweli.”

Walipotakiwa kuthibitisha wapi iwe ndani au nje ya nchi Rais alipata kutoa kauli hizo, wahariri wa RAIA MWEMA waliomba muda, wakapewa. Wakarejea na kuthibitisha kuwa hawana ushahidi huo, wakakiri kosa na kuomba radhi.

Bado Serikali inaamini kwamba Watanzania tukiufanyia mzaha upotoshaji wa taarifa na uchochezi katika zama hizi za TEHAMA amani na utulivu tulivyojivunia kwa miaka mingi vitapotea na kukaribisha maafa kama ilivyotokea kwingineko duniani.

Serikali, katika uamuzi huu, uliochukuliwa kwa mujibu wa mamlaka aliyonayo Waziri wa Habari katika kifungu cha 59 cha Sheria ya Huduma za Habari Na. 12, 2016, imetoa adhabu ndogo tofauti na ukubwa wa kosa kwa kuwa wahariri wa gazeti hili hawakufanya tashtiti, wamekiri kosa.

Hata hivyo katika suala hili tunajifunza tena mambo kadhaa kuhusu changamoto za kiwango cha weledi wa uandishi wa habari nchini kiasi inatulazimu kutoa ufafanuzi wa kina kwa faida ya umma na tasnia yenyewe; kwamba uandishi ni taaluma adhimu na yenye haki na wajibu vinavyopaswa kufuatwa na si kufanyiwa dhihaka.

Mintaarafu, mmoja wa wanasiasa waasisi wa Taifa la Marekani wanaotambulika kuwa waumini wakubwa wa uhuru wa habari, Thomas Jefferson, pamoja na kupigania sana uhuru huo, katika barua kwenda kwa rafiki yake, James Madison, wakati wa mjadala wa katiba mpya nchini humo alisisitiza wajibu wa vyombo vya habari hasa katika “….kutodhalilisha heshima ya mtu au kuharibu amani na utulivu….”

Kwa upande wake, John Stuart Mills, Muingereza anayetajwa kuwa “Baba wa Haki ya Kujieleza”ambaye katika kitabu chake mashuhuri cha “On Liberty” alitetea sana uhuru wa habari, naye alitambua umuhimu wa kutekeleza haki kwa kulinda haki za wengine alipoandika:

“The only freedom which deserves the name is that of pursuing our own good in our own way, so long as we do not attempt to deprive others of theirs, or impede their efforts to obtain it.”

Aidha, Mahatma Gandhi, Baba wa Taifa la India na mpigania uhuru na haki asiyetiliwa shaka, naye aliamini katika uhuru wa habari lakini alionya vyombo vya habari lazima vitimize wajibu wao wa kutoandika uongo na uzushi aliposema:

“I venture to suggest that rights that do not directly from duty well performed are not worth having…. The superficiality, the one-sidedness, the inaccuracy and often even dishonesty that have crept into modern journalism, continuously mislead honest men who want to see nothing but justice done.”

Mitazamo hii ya kifalsafa ya magalacha hawa mashuhuri duniani, imeenziwa na kutiliwa nguvu katika mikataba na sheria mbalimbali za kimataifa za haki za binadamu ambazo nchi yetu pia imeiridhia. Kifungu cha 19(3) cha Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kisiasa na Kiraia ambao Tanzania imeuridhia tangu mwaka 1976, kinasisitiza wajibu huu kikisema:

“3. The exercise of the rights provided for in paragraph 2 of this article carries with it special duties and responsibilities. It may therefore be subject to certain restrictions, but these shall only be such as are provided by law and are necessary:  (a) For respect of the rights or reputations of others;  (b) For the protection of national security or of public order (ordre public), or of public health or morals.

Vyombo vya habari nchini vinasisitizwa kuendelea kutekeleza wajibu huo. Serikali itaendelea kulinda uhuru wa habari unaosimama katika misingi iliyoainishwa katika nukuu hizi za wanafalsafa na sheria za kimataifa. Tunawatakia Bodi ya Wakurugenzi na wahariri wa gazeti la Raia Mwema utekelezaji mwema wa agizo hili.

Magazeti ya Tanzania leo Septemba 30, 2017
Dkt. Mwakyembe apiga marufuku matumizi ya takwimu GeoPoll