Wakati Tanzania ikiungana na dunia mwezi huu wa Oktoba kuadhimisha uhamasishaji wa afya ya akili, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Geita Gold Mining Limited – GGML, Terry Strong ameongoza wafanyakazi na wakandarasi wa kampuni hiyo kufanya matembezi ya afya ndani ya eneo la mgodi huo.
GGML imechukua hatua hiyo muhimu katika kipindi hiki cha maadhimisho hayo ili kuikumbusha jamii umuhimu kufanya mazoezi kwa ustawi wa afya ya akili, wakiongozwa na Strong, zaidi ya wafanyakazi 30 na Wakandarasi walishiriki katika matembezi hayo yaliyochukua umbali wa kilomita 5 kuzunguka eneo la mgodi uliopo mkoani Geita.
Amesema matembezi hayo yalikuwa njia ya kuufurahisha na kuuchangamsha mwili, kuboresha mahusiano ya kijamii na ustawi wa kiakili miongoni mwa wafanyakazi na kukuza urafiki na kudai kuwa AngloGold Ashanti – GGML imekuwa ikizingatia kipaumbele cha ustawi wa kiafya kwa wafanyakazi wake.
“Mwezi huu, tunapofanya matembezi haya kuamsha ari mpya ya ufanyaji mazoezi mahali pa kazi, hii inadhihirisha kuwa ndani ya GGML inathamini kujishughulisha na uwezo wa kiakili, tunajivunia kushiriki katika maadhimisho haya ya Kimataifa na kuunga mkono ustawi wa afya ya akili,” alisema.
Aidha ameongeza kuwa, “Afya ya akili inaathiri watu wengi; ni suala muhimu sana na nina furaha kuwa hapa kuliunga mkono kupitia maadhimisho haya. Ninawatakia nyinyi nyote na familia zenu heri na kuwatia moyo katika kuzingatia suala la kuangalia afya yako ya akili.”
“GGML tunaamini kuwa wafanyakazi wenye afya bora na wanaojishughulisha ni muhimu kwa mafanikio yetu kama kampuni inayojishughulisha na uchimbaji madini. Tunathamini kila mfanyakazi aliye katika timu yetu na tumejitolea kuhakikisha anakuwa katika mazingira bora kwenye nyanja zote,” alihitimisha.