Siku kadhaa baada ya Rais John Magufuli kuweka hadharani mshahara anaopokea kufuatia maombi ya muda mrefu ya viongozi wa vyama vya upinzani na wadau, gumzo hilo jana lilitua Bungeni likiwa na maombi ya ziada.

Mbunge wa viti maalumu, Upendo Peneza (Chadema) akiwa amebeba ombi lake wakati akichangi hoja katika mjadala wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa 2016/17 hadi 2021, alianza kumpongeza Rais Magufuli kwa jitihada zake na nia ya dhati anayoionesha ya kuwatumikia Watanzania akimfananisha na Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

“Kwa kweli kwa dhati kabisa nampongeza sana Rais Magufuli kwa namna anavyoonesha wazi kwamba ana dhamira ya kuwatumikia Watanzania. Kwa namna anavyokwenda ni wazi kwamba Rais Magufuli anakuwa Rais wa pili kuwa na mapenzi ya dhati kwa Watanzania baada ya Rais Nyerere [Julius Kambarage – Rais wa Serikali ya Awamu ya Kwanza].

Baada ya kumwaga sifa zake kwa Rais Magufuli, Mbunge huyo alimuomba kujipunguzia mshahara wake alioutaja pamoja na kuruhusu mshahara huo uanze kukatwa kodi kama ilivyo kwa watumishi wengine.

“Pamoja na hayo, kama anataka awe kama Mwalimu Nyerere basi ni wakati sasa wa Rais Magufuli kuchukua hatua za kujipunguzia mshahara wake na pia kuruhusu mshahara wake kukatwa kodi, hili litampa heshima kubwa sana Rais wetu,” Peneza anakaririwa.

Akijibu maombi ya Mbunge huyo kwa niaba ya Serikali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene, alisema Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haimruhusu Rais kujipunguzia mshahara anapokuwa madarakani.

“Ibara hiyo [Ibara ya 43, Ibara ndogo ya 3, Ukurasa wa 62] inasema ‘Mshahara na malipo ya Rais, havitapunguzwa wakati Rais anapokuwa bado anashika madaraka yake. Rais aliyepo sasa hawezi kujipunguzia mshahara wake yeye mwenyewe isipokuwa anapoondoka anaweza kuweka kiwango cha mshahara cha Rais ajaye,” alisema Waziri wa Tamisemi.

Magufuli kuwatumbua wanaowatetea 'aliowatumbua hadharani'
RC Lindi Amtumbua Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi