Kiungo wa Mabingwa wa Soka nchini England Manchester City, Ilkay Gundogan bado hajakubali kusaini mkataba kwa sababu akili yake ameiweka katika fainali ya Ligi Mabingwa Ulaya.
Kwa sasa mkataba wa kiungo huyo wa kimataifa wa Ujerumani umemalizika lakini mazungumzo yataanza baada ya fainali hiyo kwa mujibu wa ripoti.
Wakala wa kiungo huyo Ilhan Gundogan amethibitisha bado hawajafikia makubaliano na uongozi wa Man City na watasubiri hadi fainali ya Ligi Mabingwa Ulaya.
Awali taarifa ziliripoti Gundogun alikubali kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuendelea kukipiga Etihad msimu ujao.
Nahodha huyo wa Man City amepewa ofa na klabu mbalimbali kama Arsenal, Barcelona na AC Milan wakati mabingwa hao wa Ligi Kuu England hawana mpango wa kumuuza.
Gundogun alikuwa kinara katika fainali ya Kombe la FA dhidi ya Manchester United na kuibuka mabingwa baada ya kuichapa mabao 2-1.
Ikumbukwe Barcelona ilionyesha nia ya kumsajili Gundogun tangu kipindi cha usajili wa dirisha la kiangazi lililopita lakini ikagonga mwamba.
Arsenal inataka wachezaji wa nguvu baada ya msimu uliomalizika hivi karibuni kushindwa kutwaa taji la Ligi Kuu England baada ya kulikosa kwa miaka 19.
Arteta ambaye alikuwa na matumaini makubwa ya kutwaa taji hilo kabla ya kulikosa, sasa anapambana sokoni kuhakikisha anasuka kikosi kitakachompa taji hilo.