Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRGG) imelaani hatua zilizoripotiwa kuchukuliwa na baadhi ya wakuu wa Mkoa na wakuu wa wilaya kuwaweka selo watumishi ambao wameshindwa kutimiza majukumu yao ya kikazi.

Kwa mujibu wa tamko lililotolewa jana na mwenyekiti wa CHRGG, Bahame Nyanduga, kamisheni hiyo ilipokea ripoti ya vitendo vya baadhi ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kutoa amri za kuwakamatwa na kuwekwa selo kwa muda fulani watumishi wa umma.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa makosa ya kiutendaji yanapaswa kuchukuliwa hatua za kiutendaji kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma na sio kuwaweka jela kama watu waliofanya makosa ya jinai.

Taarifa hiyo ilitaja baadhi ya matukio ambayo imepokea ripoti zake kuwa ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kuamuru maafisa ardhi waliochelewa kufika kazini wakamatwe na kuwekwa selo kwa saa 6.

Alilitaja tukio lingine kuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma kuamuru afisa afya wa kata kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa kosa la kutosimamia ipasavyo utekelezaji wa maelekezo ya rais John Magufuli, kufanya usafi katika siku ya kumbukumbu ya Uhuru, Disemba 9.

“Kuwapa adhabu za kinidhamu ingekuwa njia bora zaidi kuliko kuwafunga jela kama wamefanya jinai,” inasomeka sehemu ya tamko hilo huku likiwataka viongozi kuzingatia haki za binadamu kama zilivyoainishwa  kwenye katiba.

Makaburi Kuwekewa Huduma ya Mtandao ya Wi-Fi
Lipumba aweka wazi jinsi Rais Magufuli alivyosaidia Kesi yake Kufutwa