Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema Yanga jana wamelitia aibu taifa kwa kucheza soka mbovu wakifungwa 1-0 na TP Mazembe ya DRC.

Yanga jana imepoteza mechi ya pili mfululizo ya Kundi A, Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufungwa 1-0, bao pekee Mereveille Boppe aliyemalizia mpira wa adhabu uliopigwa na beki Chrtistian Luyindama dakika ya 74.

Na baada ya kipigo cha hicho pili mfululizo ikitoka kufungwa 1-0 na wenyeji MO Bejaia 1-0 nchini Algeria, Hans Poppe amesema Yanga hawatafika mbali.

Akizungumza leo Dar es Salaam, Hans Poppe amesema Yanga watamaliza mkiani wa kundi hilo na hatarajii kama watapata hata sare zaidi ya kufungwa mechi zote.

“Wamecheza mpira mbovu wa kubutua butua tu kama wanavyocheza Ligi ya hapa nyumbani, kwa mchezo ule hawafiki popote, wameitia aibu tu nchi yetu, tunaonekana wote hatujui mpira,”amesema Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

“Tena Mazembe hawakufunguka jana, walicheza kwa kuwategea wakapata bao lao moja na mpira wa adhabu kwa sababu wanajua kutumia nafasi zile. Sijafurahishwa na Yanga hata kidogo, wamelitia aibu taifa,”alisema.

Yanga itahitimisha mechi zake za mzunguko wa kwanza za Kundi A kwa kucheza na Medeama ya Ghana Agosti 7 Uwanja wa Taifa pia na Hans Poppe amesema; “Hata wale wa Ghana wanakuja kujipigia tu, Yanga kelele tu na kubebwa, mpira hakuna,”.

Chanzo: Binzubeiry

Lionel Messi Aombwa Kutengea Kauli Yake
Video: Mashabiki wa TP Mazembe wakiitambia Yanga, waitangazia magoli 5 kwao