Klabu ya Njombe Mji FC inayoshiriki ligi kuu ya soka Tanzania bara kwa mara ya kwanza msimu huu, imethibitisha kuondoka kwa kocha wake Mkuu, Hassan Banyai kufuatia matokeo mabaya katika michezo mitatu.
Njombe Mji FC imepoteza michezo yote mitatu ya mwanzo za Ligi Kuu, mbili nyumbani dhidi ya Tanzania Prisons 2-0 na Young Africans 1-0 kabla ya kuchapwa 1-0 na Mbeya City Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya mwishoni mwa juma lililopita (Jana).
Kabla ya kuingia kwenye mchezo wa mzunguuko wa nne dhidi ya Ruvu Shooting Septemba 23, mwaka huu, afis ahabari wa Njombe Mji Fc Solanus Mhagama ametoa taarifa ya kuondoka kwa kocha huyo.
Mhagama amesema kwa kipindi hiki, aliyekuwa Kocha Msaidizi, Mrage Kabange ndiye ataiongoza timu hadi hapo uongozi utakapotoa tamko lingine.
Hata hivyo uongozi wa Njombe Mji FC, imemshukuru Banyai kwa mchango wake kwenye timu ikiwemo kuipandisha Ligi Kuu na kumtakia kila la heri huko aendako.
Mhagama amesema kwa sasa wanaelekeza nguvu kwenye mchezo wao ujao dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani mwishoi mwa wiki.