Bondia Hassan Mwakinyo ameondoka nchini kuelekea England, tayari kwa Pambano na Liam Smith.
Mwakinyo aliondoka Dar es salaam usiku wa kuamkia leo, baada ya changamoto zilizoelezwa huenda zingekwamisha pambano hilo, kutatuliwa mapema jana Jumatano (Agosti 31).
Mtu wa karibu wa bondia huyo amesema hadi juzi kulikuwa kuna walakini wa pambano kufanyika ama kutofanyika, lakini wahusika walikutana na kutatua changamoto ambazo zilitishia kutokuwepo kwa pambano hilo la Septemba 03.
“Alitakiwa aende tu Uingereza, mengine yatajulikana akiwa huko huko, usiku wa jana aliondoka,” amesema.
Mwakinyo aliwahi kuthibitisha kuwepo kwa changamoto ambayo ilimchelewesha kusafiri kwenda Liverpool linapopigwa pambano hilo.
“Kuna changamoto kudogo kwenye pambano langu, lakini zinatatulika,” alisema Mwakinyo.
Hata hivyo bondia huyo anatarajiwa kuwasili Uingereza mchana huu na kesho Ijumaa atapima uzito na afya tayari kupanda ulingoni Jumamosi.
“Hata kama atapigwa, atakuwa hana cha kupoteza kutokana na rekodi ya mpinzani wake,” amesema mtu huyo wa karibu wa Mwakinyo.
Ingawa Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) imedai haina taarifa za Mwakinyo kucheza Uingereza.
“Hatujampa kibali, hivyo hatujui kama atacheza au vinginevyo,” amesema rais wa TPBRC, Chaurembo Palasa.
Amesema kiutaratibu Bondia huyo alipaswa kutumia kibali cha Tanzania kwenye pambano hilo.
“Labda ana mpango wake mwingine, lakini suala la kibali analifahamu na wiki kadhaa zilizopita tulimueleza akasema atakuja, hatujui kama ameondoka na hatujui kama anapambano kwa kuwa kama msimamizi wa ngumi nchini hatujampa kibali,” amesema.