Wanamuziki Nguza Viking maarufu kama ‘Babu Seya’ na mwanae Jonson Nguza maarufu kama ‘Papii Kocha’ wamekata rufaa katika mahakama ya Haki za Binadamu Afrika (AFCPHR) wakipinga adhabu ya kifungo cha maisha gerezani iliyotolewa na mahakama ya Rufaa nchini.

Wanamuziki hao wamefungua shauri namba 006/2015 katika mahakama hiyo wakidai kuwa haki zao zilivunjwa walipopewa hukumu ya kifungo cha maisha gerezani mwaka 2004 kwa makosa ya kubaka na kunajisi watoto wa shule ya msingi Mashujaa jijini Dar es Salaam.

Wameomba kupatiwa msaada wa kisheria na mahakama hiyo kuteua jopo la wataalamu watakaotoa ufafanuzi wa hoja za kesi yao, kuachiwa huru pamoja na kulipwa fidia.

Katika kesi ya msingi, Babu Seya na mwanae wanadai kuwa shauri lao halikushughuliwa kwa kuzingatia haki za binadamu ikiwa ni pamoja na kukosewa tarehe katika tuhuma zilizopelekwa mahakamani hali wanayodai iliwapelekea kushindwa kutayarisha utetezi wao.

Wanamuziki hao pia wameiambia Mahakama hiyo ya Haki Za Binadamu Afrika kuwa mahakama iliwatia hatiani na kuwahukumu kifungu cha maisha gerezani iliegemea katika ushahidi wa upande wa mashtaka pekee bila kushirikisha ushahidi mwingine.

Walidai kuwa katika kukamatwa kwao hawakufanyiwa haki kwani hawakuelezwa sababu zilizopelekea kukamatwa kwao na pia waliteswa na kutukanwa huku wakizuiwa kufanya mawasiliano yoyote na mwanasheria wao kwa muda wa siku nne. Walisema kuwa walielezwa kuwa wanatuhumiwa kwa ubakaji baada ya kuwekwa chini ya ulinzi kwa muda.

Wanamuziki hao ambao ni raia wa Congo waliokuwa wanafanya kazi nchini wanadai kuwa mashtaka dhidi yao yalitungwa hivyo hukumu dhidi yao haikujikita katika ushahidi wenye nguvu katika sheria.

Mahakama ya Haki Za Binadamu ya Afrika inajukumu la kusikiliza rufaa kwa kesi ambazo zimekamilisha ngazi zote za kimahakama katika nchi husika barani Afrika. Mahama hiyo inayohusisha jopo la majaji kutoka katika nchi mbalimbali iko jijini Arusha, Tanzania.

 

Mashabiki Wa Spurs Walipa Kisasi Emirates Stadium
Alexandre Pato Kucheza Soka England