Kufuatia mambo kuwaendea kombo katika michezo kadhaa iliyopita ya ligi kuu ya soka Tanzania bara, viongozi wa klabu ya Stand Utd wamedhamiria kukutana na kocha Patrick Liewig ili kujua kinaga ubaga cha hali hiyo.

Mkurugenzi wa ufundi wa Stand United, Muhibu Kanu amesema wamedhamiria kufanya hivyo kutokana na mkataba wa Liewig kuwa kipengele kinachosema “endapo atapoteza mechi 4 mfululizo mkataba utavunjika” kitu ambacho tayari kocha huyo amekifanya kwani tayari ameshapoteza michezo mitano mpaka sasa.

Kanu amesema kamati ya utendaji itakutana kulimaliza jambo hilo haraka kabla mambo hayajaharibika zaidi.

Kocha Liewig anahusishwa pia kuwa na mtafaruku mkali na baadhi ya wachezaji wa kikosi chake cha kwanza (First Eleven) akiwemo mshambuliaji anayeongoza kwa kupachika magoli kwenye kikosi hicho Elias Maguri, ambaye kwa muda mrefu hajashuka dimbani.

Kocha huyo anaelezwa kuwa tabia ya visasi na wachezaji wake kiasi ambacho anaona ni bora kukosa ushindi kuliko kuwatumia katika mchezo husika, kitendo kinachotafsiriwa na uongozi kama ni kuihujumu timu.

Stand United kwa sasa inashikilia nafasi ya 7 kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 24 wakiwa na pointi 31, huku wakipoteza michezo mitano mfululizo mpaka sasa.

Kipre Tchetche Aweka Rekodi CAF
Matokeo kamili Zanzibar: Dk Shein atangazwa mshindi kwa kura hizi