Serikali nchini, imesaini Mkataba wa kwanza wa kuzalisha Umeme wa Jua wa Megawati 50 Wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga, ambao utagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 274 ambazo ni fedha kutoka Shirika la maendeleo la nchini ufaransa, AFD.
Wakati wa Hafla Hiyo Shirika la umeme nchini TANESCO limetakiwa kuandaa mapema maeneo ambao yanafaa kwa Miradi ya umeme Jua na umeme wa upepo.
Waziri wa Nishati, Januari Makamba ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati wa hafla hiyo ya utiaji Saini wa Mkataba huo na Mkandandarasi ambaye atatekeleza mradi huo na kusema kukamilika kwa Mradi huo utaandika historia na kuanisha mpango Mkakati wa Serikali kuwa na Sera ya Nishati Jadififu.
Kwa upande wake Mkuu Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme amepongeza serikali ya Awamu ya Sita kwa kuleta mradi wa Umeme wa Jua mkoani Shinyanga na kusema watahakikisha wanaulinda na kusimamia mradi huo ili ulete manufaa kwa wananchi wa Mkoa huo.
Naye Mwenyekiti, wa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini Judith Kapinga ametoa wito kwa TANESCO kusimamia na kuhakikisha mkandarasi anakamilisha mradi huo kwa muda uliopangwa.
Mbunge wa Jimbo la Kishapu Boniphace Butondo amesema mradi huo mkubwa ulikuwa unasubiriwa na wakazi wa Shinyanga kutokana na changamoto ya Umeme hivyo utaenda kutatua shida hiyo na utaleta tija kwa wakazi wa Shinyanga na utekelezaji wa Mradi unatarajiwa kuanza mwezi june 2023 na utachukua muda wa miezi 14 kukamilika kwake.