Boniface Gideon – Tanga.
Serikali nchini, imewashukuru Madaktari Bingwa 15 ambao waliowasili Mkoani Tanga mwishoni mwa wiki kujitolea kuwahudumia Wagonjwa waliopata matatizo ya viungo kupitia matukio mbalimbali hususani ya ajali huku ikitarajia kuufanya Mkoa wa Tanga kuwa kituo cha urekebishaji viungo nchini.
Shukrani hizo zimetolewa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwa Madaktari hao ambao wanaendelea na Kambi ya matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Bombo na kusema Serikali itaufanya mkoa wa Tanga kupitia Hospitali hiyo kuwa kituo cha umahiri cha upasuaji wa viungo.
Amesema, “tunashukuru kama unajua inasadikika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga -Bombo ndio ya kwanza nchini ilijengwa na wajerumani 1901 hivyo lazima tuipe hadhi yake tunakwenda kuingia makubaliano kati ya Wizara ya Afya.“
Awali akizungumza katika mkutano huo, Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo, Dkt. Mohamed Salehe alisema mpaka sasa watu watu waliojiandisha ni 250 na kati ya hao waliochunguzwa ni 196 na waliotayari kufanyiwa upasuajai ni 86 na 18 tayari wamefanyiwa upasuaji.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Japhet Simeo alisema huduma zinaotolewa za urekebishaji viungo kumfanya mtu arudi kwenye hali yake ya kawaida zina gharama ndogo ambazo wananchi huchangia ikiwemo vipimo na utaratibu wa usajili.