Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Cameroon Hugo Broos amebadili kauli na kusema anataka kubaki na timu hiyo kama mkataba wake unavyoeleza.

Broos amebadili kauli yake, baada ya siku kadhaa kupita, ambapo alikiri kuchukizwa na mwenendo wa uendeshaji soka wa nchi hiyo kutoka kwa viongozi wa shirikisho la soka Cameroon (FECAFOOT).

Broos mwenye umri wa miaka 64, amesema anapenda kuendelea kufanya kazi nchini Cameroon na anaamini mambo aliyoyaweka hadharani siku chache zilizopita yatafanyiwa kazi na viongozi wa FECAFOOT.

“Sitaondoka Cameroon,” Alisema Broos.

“Kama kuondoka nilitakiwa kufanya hivyo siku nyingi zilizopita, lakini nimeamua kuendelea kuwepo hapa, japo sitachoka kusema ukweli endapo kutakua na mapungufu ya kiutendaji.

“Naitambua kazi ninayoifanya hapa, nimeiwezesha Cameroon kutwaa ubingwa wa Afrika mwaka huu, ninataka kuendelea kufanya mambo mazuri zaidi, hasa kupata nafasi ya kushiriki fainali za kombe la dunia za 2018.”

Hata hivyo maamuzi ya mzee huyo kutoka nchini Ubelgiji yameanza kuhisiwa huenda yanatokana na kukosa nafasi ya kuwa mkuu wa benchi la ufundi la Ghana, baada ya kuomba nafasi hiyo miezi miwiwli iliyopita.

Alipoulizwa Broos kuhusu tetesi hizo alisema “Sahau kabisa kuhusu mpango wa kukosa kazi nchini Ghana, hilo halikua kusudio langu la kusema niliyoyasema juma lililopita kuhusu mapungufu ya uongozi. Ni kweli niliomba kazi ya kutaka kuwa kocha mkuu wa Ghana lakini nilitarajia majibu ya kupata ama kukosa, hivyo kukosa kwangu hakuhusiani kabisa na maamuzi ya kuendelea kubaki hapa Cameroon.”

Ghana wamemtangaza Kwesi Appiah kuwa kocha mkuu wa The Black Stars, kwa mara nyingine baada ya kuachana na Avram Grant aliyeondoka mwanzoni mwa mwaka huu.

Spika Ndugai aagiza Polisi kumkamata Halima Mdee
Antonio Conte Achekelea Kuifunga Man City