Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amemtaja mkuu wa mkoa wa Simiyu. Anthony Mtaka, kuwa ndiye mkuu wa mkoa kinara anayepiga kazi na kwamba hana mfano licha ya kupuuzwa kabla hajamteua.
Ameyasema mkoani Simiyu wakati akihutubia wananchi wa mkoa huo kwenye mkutano wa hadhara ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku 7 katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Rais Magufuli amesema kuwa, wakati anajaribu kutafuta wakuu wa Wilaya na wakuu wa mikoa ambao aliambiwa na vyombo vyake kuwa Mtaka hafai hata U-DC lakini yeye akaamua kumteua kuwa mkuu wa mkoa kwasababu anajua watu wazuri huwa wanapigwa vita sana.
”Nilipotaka kumteua niliuliza vyombo vyangu nikaambiwa hafai kabisa lakini nimeuliza ripoti ya Wakuu wa Mikoa wanaofanya kazi vizuri, wakaniletea Mtaka ndio namba moja na namba mbili ni yeye kwa kifupi hana mfano,” amesema JPM.
Hata hivyo, Rais Dkt. Magufuli ambaye atakamilisha ziara yake katika mikoa hiyo siku ya Jumatatu Septemba 10, 2018 amemtaka Mtaka kuendelea kuchapa kazi wala asiyumbishwe kwasababu yeye anajua watu wanaopigwa vita na kuwekewa maneno ya ajabu ndio wazuri.