Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amefanya mabadiliko ya makamanda wa mikoa ya kipolisi ya Tabora, Kinondoni, Lindi na Morogoro sambamba na kuwahamisha vituo vya kazi maofisa waandamizi wa jeshi hilo.
Taarifa iliyotolewa Desemba 3, 2020 na msemaji wa jeshi hilo, David Misime inaeleza kuwa aliyekuwa kamanda wa polisi Mkoa wa Kinondoni, Edward Bukombe amepelekwa makao makuu ya polisi kitengo cha picha na video na nafasi yake kuchukuliwa na Ramadhan Kingai aliyekuwa mkuu wa upelelezi Mkoa wa Arusha.
Kamishna msaidizi wa polisi Wilbroad Mutafungwa ambaye alikuwa kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro amekuwa kamanda wa kikosi cha usalama barabarani nchini na nafasi yake imechukuliwa na kamishna msaidizi mwandamizi, Fortunatus Muslim.
Aliyekuwa kamanda wa polisi mkoa wa Lindi, Stanley Kulyamo amepelekwa shule ya polisi Moshi kuwa ofisa mnadhimu wa chuo hicho na nafasi yake ikichukuliwa na Mtatiro Kitinkwi ambaye awali alikuwa ofisa mnadhimu shule ya polisi Moshi.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Tabora, Barnabas Mwakalukwa amerudishwa makao makuu ya polisi Dodoma kuwa ofisa mnadhimu katika kamisheni ya ushirikishwaji wa jamii na nafasi yake imechukuliwa na kamishna msaidizi wa polisi, Safia Shomari ambaye alikuwa ofisa mnadhimu namba moja Mkoa wa Mwanza.
Katika mabadiliko hayo Sirro amemhamisha naibu kamishna wa polisi, Mpinga Gyumi kutoka kitengo cha ufuatiliaji na tathmini makao makuu ya polisi Zanzibar na kuwa mkuu wa utawala wa rasilimali watu huku aliyekuwa mkuu wa utawala na rasilimali watu, Faustine Shilogile akipelekwa kuwa naibu mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai makao makuu ya polisi Dodoma.
Shilogile amechukua nafasi ya naibu kamishna wa polisi, Charles Kenyella ambaye amestaafu.
Naibu kamishna wa polisi, Lucas Mkondya amehamishwa kutoka idara ya maendeleo ya milki makao makuu ya polisi kuwa kaimu kamishna wa fedha na lojistiki na nafasi yake kuchukuliwa na naibu kamisha wa jeshi hilo, John Gudaba.