Iran imesema kuwa itaipiga Israel endapo itajaribu kuleta madhara yoyote kwa shughuli inayoifanya nchini Syria.
Nchi hiyo imeeleza kuwa zama za Israel kushambulia na kukimbia zilikwisha baada ya kufanya mashambulizi dhidi ya vikosi vya jeshi la Syria na maeneo yanayokaliwa na washauri wa kijeshi wa Iran nchini humo.
“Utawala wa Israel unafahamu kuwa zama za kupiga na kukimbia zimepita, na sasa hata wao wamekuwa na tahadhari kubwa,” inaeleza sehemu ya maelezo ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran, Saeed Khateebzadeh alipozungumza na vyombo vya habari hivi karibuni.
Iran imekanusha kuwa na vikosi vya kijeshi nchini Syria. Imeeleza kuwa ilituma timu ya makomando kwa ajili ya kutoa ushauri wa kijeshi kwa vikosi vya Syria na kwamba timu hiyo itakaa nchini humo kwa muda wote itakapobidi.
Uwepo wa Iran nchini Syria ni kwa ajili ya kutoa ushauri, na kama mtu yeyote ataingilia au kushambulia huu uwepo wa kiushauri, majibu yetu yatakuwa ‘kumpiga’,” Reuters wanamkariri Khateebzadeh.
Israel ambayo imekuwa ikiitaja Tehran kama tishio kubwa zaidi la usalama wake, imekuwa ikieleza kuwa imefanya mashambulizi ikilenga vikosi vya Iran na washirika wake; Iran iko nchini Syria ikimuunga mkono Rais Bashar al-Assad dhidi ya vikosi vya waasi na magaidi tangu mwaka 2012.
Jumatano wiki iliyopita, msemaji wa jeshi la Israel alieleza kuwa wameshambulia maeneo nane nchini Syria ikiwa ni pamoja na Makao Makuu ya kambi ya Iran katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Damascus ambapo huwatunza maafisa waandamizi wa Iran wanapokuwa Syria kwa ajili ya shughuli mbalimbali.