Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muunganona Mazingira), January Makamba amesema kuwa Uchaguzi wa Marudio Zanzibar uliopangwa kufanyika Machi 20 mwaka huu ni halali kisheria.

Makamba aliyasema hayo jana Bungeni Mjini Dodoma  alipokuwa akihitimisha mjadala wa kuchangia hotuba ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati akifunga mkutano wa kwanza wa Bunge la 11 mwaka jana.

Alisema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ilikaa kikao ambacho akidi ilitimia na kufanya uamuzi wa kufuta matokeo ya uchaguzi uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana, uamuzi ambao amesema ulizingatia sheria na katiba ya nchi, hivyo ni halali.

Akizungumzia kuhusu uhalali wa ZEC kufuta matokeo ya Uchaguzi huku wawakilishi kutoka Zanzibar waliochaguliwa katika uchaguzi huo wako Bungeni, alisema ZEC na NEC ni Mamlaka mbili tofauti kikatiba na kila moja ina mamlaka ya kuendesha uchaguzi na kufanya maamuzi yake bila kuingiliwa. Alisema uchaguzi huo ulifanywa na Tume mbili tofauti, madaftari mawili tofauti na hata wino ulikuwa tofauti.

Waziri huyo alisisitiza kuwa uamuzi wa kurudia uchaguzi huo ni halali kisheria hivyo wanaotaka kutafuta suluhu nje ya katiba wanafanya makosa.

Aidha, aliwatahadharisha wale wote wanaotaka kutumia mzozo wa Zanzibar kuleta vurugu visiwani humo kuwa damu ya Watanzania itawalilia.

Alisema kuwa wajibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali ni kuhakikisha wanalinda amani na utulivu katika uchaguzi wa marudio uliotangazwa na ZEC kufanyika Machi 20 mwaka huu.

Wakati Waziri Makamba akieleza hayo Bungeni, jana Baraza Kuu la Chama Cha Wananchi (CUF) lilitangaza rasmi msimamo wake kuwa chama hicho hakitashiriki katika uchaguzi huo wa marudio.

Video ya ngono yaoneshwa mazishini wakati ibada ikiendelea kupitia Runinga
Clinton kumteua Obama kuwa Jaji wa Mahakama Kuu