Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania Jenerali, Jacob John Mkunda amevitaka vikundi vya Ulinzi na Usalama vinavyoshiriki zoezi la Ushirikiano Imara 2023 kwa majeshi ya nchi za Afrika ya Mashariki kuhakikisha vinaliwakilisha vema taifa la Tanzania ili kujenga ushirikiano mzuri na nchi jirani.

Akizungumza mara baada ya ufunguzi wa zoezi hilo, Jenerali Mkunda alisema kuwa zoezi hilo liwe chachu ya kujifunza namna ya kutatua changamoto za kiulinzi na usalama katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuwa wananchi wanayategemea zaidi majeshi yao kuwapatia msaada wa ulinzi na uokozi pindi majanga yanapotokea.

Amesema, “unajua hakuna kitu kikubwa ambacho huwa kinarudisha na kujenga imani ya wananchi kwa majeshi yao kama kupewa msaada wa kijamii pindi wapatapo majanga. Imani yao kubwa hubaki kwa wanajeshi ambao ndio huwa wa kwanza kutoa msaada.”

Akizungumzia umuhimu wa ushirikishwaji wa zoezi hilo kwa taasisi na mamlaka za kiraia, Msemaji Mkuu wa Serikali Bwana Gerson Msigwa alisema kuwa huu ni wakati muafaka wa kufanya kazi pamoja kwani pindi majanga yanapotokea, mamlaka mbalimbali zinahusika kutoa utaalam wa kukabiliana na majanga hayo.

Simba SC kumng'oa STOPPER wa Cameroon
Serikali yaibua fursa miradi ya kijamii, biashara ya kaboni