Kufuatia mauaji ya Askali Polisi wanane yaliyotokea Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani, Jeshi la Polisi nchini limetangaza vita isiyokuwa na ukomo dhidi wa wahalifu.
Hayo yamesemwa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi CP. Nsato Marijani Mssanzya wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa Jeshi la Polisi limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya uhalifu huo ambapo tayari wamekwisha anza Operesheni Maalum itakayo hakikisha wahusika wote wanachukuliwa hauta stahiki.
“Niseme tu kuwa sasa umefika mwisho hatuwezi kuvumilia uhalifu wa namna hii uendelee kushamiri nchini kwetu, sisi kama Jeshi lenye dhamana ya kulinda raia na mali zao tuko imara, tutawashughulikia kikamilifu wahalifu wote, dawa ya moto ni moto,” amesema Marijani.
Aidha, ameongeza kuwa baada ya tukio hilo la mauaji, Jeshi la Polisi limechukua hatua za Kiintelijensia na Upelelezi zilizopelekea kubaini maficho ya muda ya majambazi hao ambapo Askari walifanikiwa kuwadhibiti na kufanikiwa kuwauwa majambazi wanne na kupata bunduki nne ambazo mbili kati yake zilikuwa ni zile zilizoporwa na majambazi hao katika tukio.
Hata hivyo, Katika hatua nyingine Kamishna Marijani ametangaza kuwa kuanzia sasa waendesha Pikipiki wote wa maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Rufiji Mkoani Pwani, hawataruhusiwa kufanya shughuli za bodaboda baada ya saa 12:00 jioni.