Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni jijini Dar eSalaam, limepokea msaada wa vitendea kazi ikiwemo gari moja aina ya Toyota Probox na pikipiki nne vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 30.
Vitendea kazi hivyo, vimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Kinondoni, Idd Azzan kwa lengo la kusaidia misako na doria mbalimbali za Usalama Barabarani.
Akikabidhi msaada huo, Mwenyekiti Azzan, alisema kuwa lengo la msaada huo ni kuunga mkono nguvu kazi inayofanywa na Jeshi la Polisi katika kulinda wananchi na mali zao.
Amesema, fedha hiyo pia imetokana na michango nbalimbali na kwamba wananchi pia wanatakiwa kuonesha mshikamano wakati jeshi likiendelea na shughuli zake za kulinda usalama wa wananchi wake.
Akipokea msaada huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, ACP. Mtatiro Kitinkwi amesema “Mkoa wa Kipolisi Kinondoni unatoa shukrani za dhati kwa Kamati ya Usalama Barabarani ya Mkoa huo kwa msaada iliyowakabidhi.”
Amesema, msaada huo umekuja wakati muhafaka kwani utasaidia katika kurahisisha utendaji kazi za usalama barabarani, zikiwemo kukwamua foleni, kuzuia na kukamata makosa hatarishi ambayo yanaweza kusababisha ajali.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni linawasihi madereva wote wa vyombo vya moto na watumiaji wengine wa barabara kutii na kufuata Sheria na Kanuni za usalama barabarani pamoja na Sheria za Nchi kwa ujumla,” ameongeza Kamanda Kitinkwi.
Aidha, ametoa wito kwa madereva, wamiliki wa vyombo vya moto kutengeneza vyombo vyao vya moto mara vinapokuwa na hitilafu, na kufanya ukaguzi wa kila mara ili kuhakikisha vyombo hivyo vinakuwa katika hali nzuri.