Jeshi nchini Afrika ya Kusini limeingilia kati mgomo wa Wahudumu wa afya kwa kupeleka Madaktari wake katika hospitali kadhaa za umma, ili kupunguza madhara na vifo, huku Serikali ikisema hali hiyo ilisababisha vifo vya watu kadhaa.
Msemaji wa Jeshi hilo, Phillip Makopo amesema, “Tumepokea ombi kutoka kwa Waziri wa Afya kusaidia katika mgomo unaoendelea na kuhakikisha kuwa huduma za afya zinafanya kazi bila usumbufu wowote.”
Waziri wa Afya wa Afrika Kusini, Joe Phaahla amesema takriban wagonjwa wanne wamefariki na kwamba vifo vyao vinaweza kuhusishwa moja kwa moja na mgomo huo, ambapo wiki iliyopita, wagomaji walizuia watu kufika katika hospitali mbalimbali.
Machi 13, 2023, Askari wanne wa Jeshi la nchi hiyo walionekana wakiwa wamekaa karibu na Hospitali ya Thelle Mogoerane iliyopo kusini mashariki mwa Johannesburg, huku polisi wakishika doria kwenye lango la kuingilia.