Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed amevipa vikosi vya jimbo la Tigray muda hadi siku ya Jumatano ili kusalimu amri, kabla ya vikosi vyake kuanza operesheni ya kijeshi katika mji mkuu wa jimbo hilo, Mekelle.
Kwenye ujumbe alioandika katika ukurasa wake wa Twitter, Abiy amewataka wapiganaji hao kusalimu amri kwa amani ndani ya muda wa saa 72, akisema imefikia hatua ya kutorudi nyuma.
Chama tawala katika jimbo hilo TPLF, kimesema wanajeshi wake wamekuwa wakichimba mahandaki na wanasimama imara dhidi ya vikosi vya Ethiopia.
Siku moja baada ya Abiy kutoa amri hiyo, Umoja wa Mataifa umeihimiza Ethiopia kuhakikisha raia wanalindwa.
Maelfu ya watu wameuawa tangu machafuko yalipoanza kati ya vikosi vya serikali ya shirikisho ya Ethiopia na jeshi la jimbo la Tigray, na kusababisha zaidi ya wahamiaji 30,000 kukimbilia nchi jirani ya Sudan.
Kupitia ukurasa wa Twitter, jopo kazi la serikali kuhusu masuala ya dharura limesema vikosi vyao vimeonyesha viwango vya juu vya kuwalinda raia dhidi ya kujeruhiwa, wakati wa operesheni yao ya kuhakikisha usalama katika jimbo la Tigray.
Awali, msemaji wa jeshi la Ethiopia Dejene Tsegaye, alisema wanajeshi wa Ethiopia wanapanga kuuzingira mji wa Mekelle kwa vifaru na wanaweza kuushambulia ili kuwalazimisha wapiganaji wa Tigray kusalimu amri.