Operesheni ya uhakiki wa wanafunzi wa elimu ya juu wanaofaidika na fedha za Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu iliyoanza jana tayari imebaini kuwepo madudu ya wanafunzi hewa na marehemu ambao wameendelea kuombewa na kupata fedha za mikopo.

ndalichako

Profesa Joyce Ndalichako

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amebainisha hayo leo katika mkutano na waandishi wa habari alipokuwa akitolea ufafanuzi sakata la ucheleweshwaji wa fedha za mafunzo kwa vitendo (field) kwa  wanafunzi wa elimu ya juu nchini.

Profesa Ndalichako amesema kuwa walianza zoezi hilo kwa kuviomba vyuo hivyo kuwasilisha taarifa za wanafunzi waliofukuzwa, walioahirisha masomo pamoja na walioacha vyuo ndipo walipokutana na madudu hayo.

“Kwa uchambuzi ambao tulikuwa tumeanza kufanya jana kwenye vyuo viwili, tumebaini kwamba wapo baadhi ya wanafunzi ambao ni marehemu lakini wameombewa fedha kwa ajili ya field,” Profesa Ndalichako alisema.

“Wapo wanafunzi ambao chuo chenyewe kimeleta taarifa tena taarifa ambazo ni za hivi karibuni. Waliwasilisha taarifa zao tarehe 20 mwezi wa sita wakiwa wanaonesha kwamba baadhi ya wanafunzi walikuwa wamefukuzwa tangu mwaka 2013/14 lakini majina yao yapo wameombewa mikopo,” aliongeza.

Alisema kuwa hawatatoa pesa za mikopo hiyo hadi watakapokamilisha uhakiki wa majina ya wanafunzi husika kwani Serikali inapoteza fedha nyingi kuwalipa wanafunzi wasiokuwepo au wasio na sifa.

Katika hatua nyingine, Profesa Ndalichako amesema kuwa kati ya wanafunzi 7805 walioondolewa kwa muda katika Chuo Kikuu cha Dodoma, ni wanafunzi 382 pekee walio na sifa za kuendelea na masomo yao katika chuo hicho na kwamba ndio watakaorudishwa.

Wizara Ya Maliasili Na Utalii Yatakiwa Kujipanga
Ndalichako Atoa Majibu ya Waliofukuzwa Udom Wenye Sifa ni 382 tu