Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza kulipa kisasi kwa wote waliohusika kwenye shambulio lililotokea uwanja wa ndege wa Kabul nchini Afghanistan.
Biden amesema hayo baada ya shambulio hilo kuua watu 90 wa Afghanistan miongoni mwao wakiwemo wanajeshi 13 wa Marekani huku watu 140 wamejeruhiwa kwenye shambulio hilo.
Aidha Msemaji wa Makao Makuu ya jeshi la Marekani Pentagon, John Kirby amesema kuwa mlipuko mmoja umetokea karibu na lango la Abbey la kuingilia uwanja wa ndege wa Kabul na mlipuko wa pili umetokea jirani kabisa na hoteli ya Baron iliyopo karibu na uwanja huo.
“Askari 13 wa Marekani ni miongoni mwa waliouawa katika mashambulio hayo”. Amesema Kirby.
Hili ni shambulizi kubwa la kwanza kutokea mjini Kabul tangu rais Ashraf Ghani aitoroke nchi na mji mkuu huo wa Afghanistan kudhibitiwa na kundi la Taliban mnamo tarehe 15 Agosti.