Kiungo na nahodha wa timu ya taifa ya Nigeria, John Mikel Obi ameomba kuachwa kwenye kikosi cha timu hiyo, ambacho kitacheza mchezo wa kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika (AFCON 2019), dhidi ya Libya mwezi huu.
Taarifa iliyothibitishwa na shirikisho la soka nchini Nigeria (NFF), Obi aliwasilisha ombi la kutaka kuachwa katika kipindi hiki, ili apate nafasi ya kupata ahuweni ya majeraha yaliyowahi kumsumbua siku za nyuma.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 31, hajawahi kuitumikia timu ya taifa ya Nigeria, tangu ilipotolewa kwenye fainali za kombe la dunia nchini Urusi mwezi Juni mwaka huu.
Hata hivyo Obi ambaye kwa sasa anaituikia klabu ya Tianjin TEDA, inayoshirili ligi kuu ya soka nchini China, anatarajiwa kurejea kikosini mwezi ujao, kwa ajili ya mchezo dhidi ya Afrika kusini.
“Mikel ameomba kuachwa katika kipindi hiki, ili apate nafasi ya kupumzika, kutokana na majeraha yaliyokua yakimsumbua kwa majuma kadhaa, tumeheshimu ombi lake,” Msemaji wa timu ya taifa ya Nigeria Toyin Ibitoye, aliliambia shirika la utangazaji la Uingereza BBC.
“Tunamtegemea mwezi ujao, tunaamini atakua Fit kucheza katika kikosi cha Super Eagles, ambacho kina kiu ya kushiriki fainali za Afrika mwakani.”
Wakati huo huo kocha mkuu wa timu ya taifa ya Nigeria Gernot Rohr, amefanya mabadiliko kwenye kikosi chake kwa kuwaita wachezaji watatu, ambao hawakuwepo wakati wakipambana na Sheli Sheli mwezi uliopita.
Watatu hao walioitwa kikosini tayari kwa mchezo dhidi ya Libya, ni Kelechi Nwakali, Simeon Nwankwo na Joel Obi.
Naye mshambuliaji wa klabu ya Watford Isaac Success, ametajwa kwenye kikosi cha Nigeria, kufuatia uwezo na umahiri mkubwa naoendelea kuuonyesha katika ligi ya England, sambamba na mshambuliaji wa Levante ya Hispania Moses Simon na beki wa klabu ya Bursaspor ya Uturuki Shehu Abdullahi.
Kikosi cha Nigeria pia kitachagizwa na hatua ya kurejea kwa mshambuliaji wa klabu ya Arsenal ya England Alex Iwobi na mabeki William Troost-Ekong na Ola Aina, baada ya kukosekana katika mchezo wa mwezi uliopita dhidi ya Sheli Sheli, ambao walikubali kufungwa mabao matatu kwa sifuri.
Nigeria watakua wenyeji wa Libya katika mji wa Uyo Oktoba 13, na siku tatu baadae watasafiri hadi Stade Taïeb Mhiri mjini Sfax, Tunisia, kucheza mchezo wa marudio dhidi ya Libya.
Kikosi cha Nigeria kilichotajwa kwa ajili ya mchezo dhidi ya Libya:
MAKIPA: Francis Uzoho (Elche FC/Spain), Ikechukwu Ezenwa (Enyimba, Nigeria) na Daniel Akpeyi (Chippa United/South Africa)
MABEKI: Ola Aina (Torino FC/Italy), Abdullahi Shehu (Bursaspor FC/Turkey), Semi Ajayi (Rotherham United/England), Brian Idowu (Lokomotiv Moscow/Russia), Chidozie Awaziem (FC Porto/Portugal), William Ekong (Udinese FC/Italy), Leon Balogun (Brighton and Hove Albion/England), Kenneth Omeruo (CD Leganes/Spain) na Jamilu Collins (SC Padeborn 07/Germany)
VIUNGO: Ogenyi Onazi (Trabzonspor FC/Turkey), Wilfred Ndidi (Leicester City/England), Oghenekaro Etebo (Stoke City FC/England) na John Ogu (Hapoel Be’er Sheva/Israel)
WASHAMBULIAJI: Ahmed Musa (Al Nassr FC/Saudi Arabia), Kelechi Iheanacho (Leicester City/England), Moses Simon (Levante FC/Spain), Henry Onyekuru (Galatasaray SK/Turkey), Odion Ighalo (Changchun Yatai/China), Alex Iwobi (Arsenal/England), Samuel Kalu (Bordeaux/France) na Isaac Success (Watford/England).