Jonas Malheiro Savimbi ni moja ya Wanasiasa na Wapigania Uhuru katika moja ya mataifa yaliyopo kusini mwa Afrika yaani Angola aliyezaliwa Agosti 3, 1934 eneo la Moxico Munhango lililopo jimbo la Bie Angola, wakati Wakoloni Wa Kireno wakilitawala Taifa hilo.
Kihistoria yeye ni mtoto wa Mfanyakazi wa Reli ya Benguela, baba yake alikuwa ni Mkuu wa kituo cha Reli na Kitaaluma alisoma shule za kidini za misheni, ambazo kwa wakati huo zilikuwa ngumu sana kuwapokea watu weusi.
Lakini kutokana na ndugu yake Savimbi kuwa mmoja wa machifu wa kabila la Ovimbundu, basi ikawa rahisi kufanya Urafiki na wamishionari wa Roman Katoliki na kufanikiwa kuhitimu masomo yake ya awali na baadaye alipata ufadhiri wa kimasomo na kwenda ng’ambo.
Alisoma taaluma ya madawa (Udaktari) katika Chuo Kikuu cha Lisbon nchini Ureno mwaka 1958-1960, Chuo Kikuu cha Fribourg mwaka 1961- 1964 na baadaye alijiunga na chuo kikuu cha Lausanne nchini Uswizi huku akibobea katika Sayansi ya Siasa mwaka 1964-1965, huku akiweza kuongea kwa ufasaha lugha saba tofauti duniani.
Huku akiwa masomoni huko Lisbon miaka ya 1950 alianza kuupinga utawala katili wa Kireno nchini Angola na mwaka 1961 alipata kiu ya kuwa Mwanaharakati wa kulikomboa Taifa la Angola kutoka katika makucha ya wakoloni wa Kireno, hivyo akajiunga na moja ya kundi la wapigania Uhuru la Popular Union of Angola – UPA.
Baadaye kundi hilo likaitwa National Liberation Front Of Angola – FNLA, lililokuwa chini ya Uongozi Wa Holden Roberto na lijiunga nalo kama mpiganaji wa kawaida asiye na ujuzi mkubwa katika mapambano ya Msituni.
Mwaka 1965, alikwenda China kupata mafunzo makubwa ya kijeshi akibobea mapambano ya vita vya Msituni ambapo alikutana na kiongozi Wa Taifa la Uchina Mao Tse Tun, Viongozi wa Kijeshi na wanasiasa wa Chama cha Kikomunisti ambapo wote kwa pamoja walimpa mbinu mbalimbali za kukabiliana na vita vya Msituni.
Aliporejea nchini kwake, kwa miaka zaidi ya 30, Savimbi alipigana akiwa Msituni na hii ilimfanya kuonekana Mpiganaji hodari wa vita vya Msituni ingawa aliuawa kinyama badaye Karibu na eneo moja la Lucusse katika jimbo maarufu la Moxico Nchini Angola.
Alikuwa ni mwanasiasa na Kiongozi wa muda mrefu Wa Kikosi cha Askari wapigania Uhuru wa Msituni wa Taifa hilo lililojinyakulia Uhuru kwa mtutu Wa Bunduki, ikisaidiwa na mataifa yaliyokuwa mstari wa mbele kama Tanzania, Zimbabwe nk, huku akitajwa kama muasi hatari zaidi kuwahi kutokea kwenye karne ya 19.
Baada ya Uhuru wa Angola mwaka 1975, yeye aliendelea kupigana na Serikali ya Angola kwani katika fikra zake aliamini bado watu Wa Angola hawajapata Uhuru kamili na aliwahi kaririwa na Gazeti moja la Reader’s Digest akisema “Kutoka kwa Mao na Wakoministi nilijifunza namna ya kupigana na kushinda Vita vya Msituni.
Aidha Savimbi alibainisha kuwa, nilijifunza kuendesha Uchumi au Taifa, Utajiri wa Taifa hutengenezwa na hatua zinazochukuliwa na watu Binafsi na hii ilikuwa ni baada ya mafunzo ya kijeshi huko China aliporejea nyumbani na kuendeleza harakati zake za ukombozi Wa Taifa la Angola.
Taratibu Savimbi alianza kuwahamasisha watu wa jamii ya Ovimbundu ambao ni robo tatu ya nchi hiyo kuanza kujitambua na kupigania Uhuru wao kutoka kwa Mkoloni wa kireno ambapo Machi 13, 1966 baada ya kuona kundi la FNLA ni dhaifu sana halifikii malengo yake aliamua kujiengua au kujitoa.
Akafanikiwa kuunda kundi la wapigania uhuru lijulikanalo kama National Union for the Total Independence of Angola -UNITA, na kuanza kuendeleza ndoto yake ya kuung’oa utawala Wa Kireno lakini udhaifu wa FNLA ulitokana na mapigano yake dhidi ya watawala wa Kireno kuanzia nchini Zaire kwa sasa DRC.
Kutokana na sababu kuwa FNLA walikuwa dhaifu sana na kiu yake Savimbi ilikuwa ni kuanzisha mapambano kutokea katika ardhi ya Angola na si Zaire (sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo -DRC), na Savimbi alishirikiana na Antonio da Costa Fernandez kuunda UNITA katika eneo lijulikanalo kama Muangai jimbo la Moxico.
Desemba 25,1966 pambano la kwanza La UNITA lilifanywa dhidi ya Wakoloni Wa Kireno na Savimbi ndiye kiongozi wa wapiganaji wa Msituni aliyesalia nchini Angola huku akipigana na Wareno kwani alikuwa amejiamini vilivyo dhidi ya utawala katili na dhalimu wa Wareno.
Ikumbukwe pia UNITA ilianza kama kikundi cha kikomunisti kufuatana na itikadi ya Mao Zedong lakini uadui kati ya Wakomunisti wa Uchina na Urusi ulionekana katika mashindano ya UNITA dhidi ya MPLA (kwa Kireno – Movimento Popular de Libertação de Angola – Partido do Trabalho) iliyosaidiwa na Urusi.
Na ilipofika Novemba 10, 1975 Taifa la Angola lilipata Uhuru wake kutoka kwa Wareno na hatimaye harakati za kutaka kuunda Serikali huru ya Angola zikaanza na chama cha MPLA kikiwa ni miongoni mwa vyama vilivyokuwa vikipigania Uhuru dhidi ya Wareno kiliunda Serikali mpya rasmi lakini Savimbi bado aliendelea kuipinga.
Baadaye Savimbi alipata usaidizi kutoka kwa maadui wote wa MPLA bila kujali itikadi. UNITA ilipata misaada toka serikali mbalimbali duniani ili kuiondoa madarakani serikali ya MPLA, alikuwa akipata misaada ya fedha na silaha toka serikali za Marekani, China, Afrika Kusini, Ivory Coast, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (wakati huo ikijulikana kama Zaire), Moroko, n.k.
Serikali ya Angola ilikuwa ikipata misaada toka Urusi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kijerumani, Kuba, na Nicaragua hata hivyo, Savimbi aliuawa vitani Februari 22, 2002 na Askari wa jeshi la Angola katika eneo la Moxico ambako ndiko alikozaliwa, halafu muda mfupi baadaye UNITA na MPLA zilikubaliana kusimamisha mapigano.
Hata hivyo, kuuawa kwake kulikuja baada ya kunusurika na mashambulizi ya mara kadhaa ambapo alitangaziwa kuwa amekufa zaidi ya mara 15, lakini haikuwa hivyo na hata alipouawa kwa kupigwa risasi risasi zaidi ya 10 zilizompata sehemu mali mbali kichwani, kooni, miguuni ila hakufa kirahisi mpaka pale alipoanza kujibu mashambulizi ndipo hali yake ikawa mbaya, akafariki.
Hapo ndipo UNITA ikachukua nafasi ya chama cha upinzani. Hata hivyo taratibu za kidemokrasia zilichelewa hadi chaguzi za miaka 2008 na 2012 na toleo la katiba mpya la mwaka 2010 huku Savimbi akiacha alama ya kupendwa na wanadiplomasia wa nchi mbalimbali ikiwemo Marekani ambao walikuwa na manufaa na migogoro ya Angola.