Licha ya kuibuka na ushindi wa mabao mawili kwa moja katika mchezo wao wa mwisho dhidi ya Real Madrd, kwenye ziara ya nchini Marekani, meneja wa Man Utd Jose Mourinho amesema hajajifunza chochote.
Mourinho amesema maneno hayo alipozungumza na waandishi wa habari mara baada ya mchezo wa Real Madrid uliochezwa usiku wa kuamkia leo, ambapo amesisitiza bado kuna kazi ya kufanya kabla ya kuanza harakati za kuwania taji la England msimu wa 2018/19.
Meneja huyo kutoka nchini Ureno, amesema ziara yao ya Marekani haijakinufaisha chochote kikosi chake ambacho kwa msimu ujao kinatajwa kuwa sehemu ya timu zinazopewa nafasi ya kutwaa ubingwa.
“Sijajifunza lolote katika ziara hii,” Alisema meneja huyo. “Ninafahamu nini walichokifanya Ander Herrera, Juan Mata na Alexis Sanchez, lakini sijaridhishwa na mlichokiona.
“Ninatambua suala la kuja katika ziara hii na kikosi kilichosheheni vijana wengi huenda ilikua kikwazo kwangu na kwa wengine, lakini vijana wamejitahidi kujifunza mambo kadhaa na kucheza michezo ya kirafiki, japo ninarudia kusema hakuna nilichojifunza kwangu mimi kama meneja.
“Tunahitaji kutengenza wigo wa kupambana kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi, tunahitaji kuangaliwa kivingune tofauti na sasa.”
Katika mchezo dhidi ya Real Madrid mabao ya Man Utd yalifungwa na Alexis Sanchez na Ander Herrera dakika ya 17 na 28 huku bao la mabingwa wa barani Ulaya likikwamishwa wavuni na mshambuliaji Karim Benzema dakika ya 45.
Kabla ya mchezo dhidi ya Real Madrid, Man Utd walicheza dhidi ya Liverpool na kukubali kibano cha mabao manne kwa moja, mchezo mwingine ulikua dhidi ya AC Milan uliomalizika kwa sare ya bao moja kwa moja na Mashetani Wekundu walishinda kwa penati tisa kwa nane.
Klabu ya San Jose Earthquakes nayo ilipambana na Man Utd katika mchezo wa kirafiki huko Marekani na kuambulia matokeo ya sare ya bila kufungana, huku Club America ikiwatunishia msuli wababe hao wa Old Trafford kwa kutoka sare ya bao moja kwa moja.
Agosti 05 kikosi cha Jose Mourinho kitashuka tena dimbani kucheza mchezo wa mwisho wa kirafiki katika kipindi hiki cha maandalizi dhidi ya FC Bayern Munich ya Ujerumani, na Agosti 10 kitaanza harakati za kusaka taji la England kwa kucheza dhidi ya Leicester City.