Baadhi ya maduka katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam, yameendelea kufungwa kufuatia mgomo wa wafanyabiashara wanaopinga rushwa na malimbikizo ya kodi wanayotozwa na Mamlaka ya Mapato nchini Tanzania – TRA.
Mgomo huo ambao ulifanyika jana Jumatatu (Mei 15, 2023), umekuwa na mgawanyiko miongoni mwa wafanyabiashara ambao baadhi yao wameelezea msimamo wa kuendelea na mgomo mpaka watakapo kutana na rais Samia Suluhu Hassan, ili aweze kutatua changomoto zinazowakabili.
Licha ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amosi Makala na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuzungumza na wafanyabiashara hao, bado baadhi yao wamedai kuwa wataendelea na mgomo huku Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kariakoo, Martin Mbwana akisema hali hiyo inasababishwa na kikundi cha watu wachache wenye maslahi binafsi.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Soko Kuu la Kariakoo, Martin Mbwana.
Hata hivyo, amesema kilio chao kama wafanyabiashara ilikuwa ni kusikilizwa na Rais Samia na katika kuonesha amewasikia alimtuma Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kuongeza kuwa, “shida ni kikundi cha watu wachache wanaoonekana kuwa na manufaa na mgomo huo huku akieleza kuwa ameomba msaada kwa vyombo vya usalama.
Wafanyabiashara hao wamekuwa wakitumia makundi ya watu katika mitandao ya kijamii kuhamasisha kuendeleza mgomo, huku wakichapisha mabango ya kutaka kuonana na rais, wakilalamikia kamatakakamata ya wafanyabiashara, utoaji wa risiti za kielektroniki na mapungufu ya sheria mpya ya usajili wa stoo.