Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetakiwa kujitathmini kutokana na kuonekana kwa watu kukwepa kulipa kodi na kuamua kutumia wamachinga na wafanyabiashara wadogo kuwauzia bidhaa zao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema hayo leo Desemba 2, 2018 wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi wa uboreshaji wa huduma za maji safi na maji taka katika kijiji cha Kimnyaki mkoani Arusha.
Rais Magufuli amesema baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wamekuwa na tabia ya kutumia wamachinga kuuza bidhaa zao ili wasilipe kodi.
“Mnaweka viwango vikubwa ambavyo havilipiki jambo ambalo linafanya wafanyabiashara kukwepa, hivyo ni bora kuweka viwango vidogo vinavyolipika na wengi kuliko kiwango kikubwa kinacholipwa na watu wachache,” amesema.
Amesema kuwa baadhi ya kodi zinazokusanywa na TRA ni za kuudhi kwani licha ya kuwa aliwaagiza kukusanya kodi kila sehemu ila sio za dhulma.
Aidha, Rais Magufuli amewataka wamachinga kutumia vizuri fursa ya kufanya biashara kila sehemu waliyopewa ila sio katika kukwepa kodi.
Amesisitiza kuwa “Wafichueni watu wenye tabia ya kukwepa kodi ili wasiwaharibie na muwe mnatoa elimu na sio kupeleka Polisi kuwakamata wananchi wanaposhindwa kulipa kodi,” amesema.