Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa amemuapisha Mabula Misungwi Nyanda, kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania – TAWA, katika hafla iliyofanyika Hifadhi ya Urithi wa Dunia Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara, Mkoani Lindi.
Akizungumza baada ya hafla ya uapisho na uvalishaji wa cheo kipya cha kijeshi kwa Kamishna wa Uhifadhi Machi 14, 2023, Mchengerwa amempongeza Kamishna Mabula na kumtaka kuendelea kutekeleza yale mazuri yaliyofanya ateuliwa kuiongoza TAWA.
Amesema, “yale mazuri uliyoyafanya ndani ya TAWA hadi kukupa sifa ya kuteuliwa uyaongeze zaidi na yawe chachu katika kuongeza usimamizi wa rasilimali ya Wanyampori na malikale” amesema Mhe. Mchengerwa.
Aidha, Mchengerwa pia ameagiza watumishi wote kuwa waadilifu na waongeze juhudi katika ufanyaji kazi ili kuhakikisha malengo ya Serikali kwa kupitia TAWA yanafikiwa na kutoa rai kwa wananchi kuheshimu sheria na kanuni za uhifadhi zilizowekwa na Serikali, ili kuepusha migogoro baina ya wahifadhi na wananchi.
Awali, akitoa salamu za ukaribisho, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA, Mej.Gen (Mstaafu) Hamis Semfuko alimshukuru Waziri Mchengerwa kwa kumthibitisha Kamishna Mabula ndani ya mufa mfupi tangu ateuliwe na Rais Dkt. Samia, kuiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii.
Kwa upande wake, Kamishna Mabula alimuahidi Waziri Mchengerwa kutekeleza yote aliyoyaagiza sambamba na kuchapa kazi kwa bidii na kwa ubunifu ili kuhakikisha malengo ya Taasisi na Wizara yanafikiwa huku akiwashukuru Maafisa na Askari wote kwa ushirikiano waliompa wakati anakaimu nafasi hiyo.