Uongozi wa klabu ya Ruvu Shooting umetoa ufafanuzi wa suala la kuondoka kwa aliyekua kocha wao Tom Alex Timam Olaba, katika kipindi hiki cha kuelekea kuanza kwa michezo ya ligi kuu ya soka Tanzania bara, msimu wa 2016/17.

Mapema hii leo, uongozi wa klabu hiyo inayomilikiwa na jeshi la kujenga taifa JKT, ilitoa taarifa za kuachana na kocha huyo kutoka nchini Kenya, bila kutoa sababu maalum hali ambayo ilizua tafrani na maswali mengi miongoni mwa wadau wa soka nchini.

Dar24.com imezungumza na afisa habari wa Ruvu Shooting Masau Bwire kwa lengo la kutaka kufahamu sababu za kuondoka kwa Tom Olaba, ambaye aliwasaidia kurejea katika mshike mshike wa ligi kuu ya soka Tanznaia bara wakitokea ligi daraja la kwanza msimu wa 2015/16.

Masau Bwire alisema kuondoka kwa kocha huyo kumetokana na kanuni za ligi kuu kutomtambua, kwani anakosa sifa za kuwa na leseni daraja la pili, ambazo zinamnyima nafasi ya kukaa kwenye benchi la Ruvu Shooting ambayo msimu ujao itashiriki ligi kuu ya soka Tanzania bara.

Masau aliongeza kuwa walitamani kuendelea kufanya kazi na kocha huyo, lakini wameona kuna haja ya kuachana nae kwa wema, kutokana na sababu hiyo, huku akiwasisitiza mashabiki wa Ruvu Shooting kupuuza taarifa ambazo huenda zitajitokeza kuhusu kuondoka kwa Olaba.

“Tulikua hatuna budi kuachana nae, kutokana na kukosa sifa za kuwa na leseni ya ukocha daraja la pili la ukocha, hivyo kwa mujibu wa suala hilo tumeona ni bora kumruhusu aondoke.” Alisema Masau Bwire

Tom Olaba ana leseni ya ukocha daraja la tatu ambayo inatambuliwa na shirikisho la soka barani Afrika CAF, na kwa hapa Tanzania leseni hiyo inaishia katika ukufunzi wa klabu za ligi daraja la kwanza.

Hata hivyo Masau Bwire alisema tayari uongozi wa Ruvu Shooting umeshatangaza kujaza nafasi ya Tom Olaba, kwa kumpandisha aliyekua kocha msaidizi Seleman Mtungwe kuwa mkuu wa benchi la ufundi.

Alisema Mtungwe ametimiza vigezo vya kuwa mkuu wa benchi la ufundi, baada ya kuhudhuria na kumaliza kozi ya ukocha daraja la pili, tena kwa kugharamikiwa na uongozi wa klabu hiyo ya Mlandizi mkoani Pwani.

“Tunamuamini kwa kiasi kikubwa Seleman Mtungwe, ataweza kutimiza jukumu lake ipasavyo, kwa sababu amekua hapa kwa muda mrefu kama kocha msaidizi na amejifuza mengi kutoka kwa makocha karibu wote tuliowahi kuwa nao.” Alisema Masau Bwire

Olaba alianza kuifundisha Ruvu Shooting msimu mwaka 2013/14 na aliikuta timu hiyo ikiwa na point 17, na mwishoni mwa msimu huo alimaliza akiwa katika nafasi ya 5 kwa kufikisha point 35.

Msimu wa 2014/15, Olaba haikufanya vizuri katika michezo ya ligi kuu, hali ambayo ilipelekea Ruvu Shooting kushuka daraja ikiwa na jumla ya pointi 29.

Hata hivyo pamoja na kushuka daraja, Olaba alikubali kuendelea na kazi yake, kwa kuiongoza Ruvu Shooting katika michezo ya ligi daraja la kwanza msimu wa 2015/16 akiahidi kuipandisha daraja, ahadi ambayo aliitekeleza.

Dar esalaam na Dodoma inaongoza kwa Vitendo Vya Ushoga - Ummy Mwalimu
Wanafunzi Watakao hakikiwa vyuo Vikuu kupata Fedha za mafunzo