Uongozi wa Klabu ya Simba SC umeanza kuboresha mikataba ya wachezaji wao inayotamatika mwishoni mwa msimu huu kabla ya kuanza kushusha vifaa vipya, kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa.
Hii ni baada ya msimu huu tena kutoambulia taji lolote huku wakishindwa kufikia lengo lao la kutinga Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, walilokuwa wamejiwekea, jambo ambalo limewaamsha na kuahidi usajili mkubwa.
Tayari Young Africans imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu, hivyo Simba SC haina nafasi tena ya kubeba taji hilo huku ikiondoshwa kwenye Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ katika hatua ya nusu fainali na Azam FC, lakini pia ikikomea Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutolewa na mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Wydad Casabanca ya Morocco kwa mikwaju ya penalti 4-3, hiyo ikitokana na kila timu kushinda bao 1-0 nyumbani.
Hata hivyo, Simba SC itakuwa timu pekee katika Ukanda wa Afrika Mashariki, itakayoshiriki michuano mipya na mikubwa zaidi kwa ngazi ya klabu Afrika, Super League, inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Oktoba mwaka huu ikishirikisha klabu nane kubwa, jambo ambalo wamesema wanataka kujipanga mapema.
Ofisa Mtendaji wa Simba SC Imani Kajula, amesema watafanya usajili mkubwa wa wachezaji wenye viwango vya hali ya juu kuelekea msimu ujao na wakati akitoa kauli hiyo, jana beki wa kulia, Shomari Kapombe, amesema yupo kwenye mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya.
Katika mahojiano yake na Meneja Habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally, Kapombe amesema mkataba wake unafika ukingoni mwishoni mwa msimu huu na tayari wasimamizi wake wameanza mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo.
Kapombe amesema: “Kwa sasa sifikirii kwenda klabu yoyote zaidi ya kubaki Simba, mkataba wangu unaelekea ukingoni na wawakilishi wangu wanaendelea na mazungumzo na viongozi, naamini tutafikia makubaliano mazuri,” amesema.
Endapo mazungumzo hayo yakikamilika, Kapombe atakuwa mchezaji wa pili kuongeza mkataba mpya baada ya beki kisiki wa kati wa timu hiyo, Henock Inonga, kufanya hivyo Desemba mwaka jana.