Rais wa Kenya, William Ruto amemfuta kazi Katibu Mkuu anayesimamia afya ya umma na kuvunja bodi nzima ya taasisi ya kununua vifaa vya matibabu kutokana na kashfa ya ufisadi.
Hatua hiyo, inahusisha zabuni ya usambazaji wa vyandarua vya thamani ya takribani dola milioni 27 vilivyotolewa na wafadhili kwa lengo la kukabiliana na mbu wanaosababisha malaria.
Mamlaka ya Ugavi wa Dawa nchini – KEMSA, iliagizwa kununua zaidi ya vyandarua milioni 10 ambavyo vingetolewa kwa watu walio na kipato cha chini katika kaunti kadhaa zinazokabiliwa na ugonjwa wa malaria.
Hata hivyo, Global Fund ilighairi zabuni hiyo ikiishutumu KEMSA kutoa upendeleo kwa kampuni moja ambayo nyaraka zake hazikuwa katika mpangilio na kuwafungia nje wengine.