Jumla ya watu 23,495 ambao ni sawa na asilimia 2, wamekutwa na virusi vya Ukimwi ‘VVU’ kati ya watu 948,094 waliopima ugonjwa huo nchini Ghana kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2022, kituambacho kimeshtua umma wa nchi hiyo na mataifa jirani.
Meneja Programu wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa ya Ngono na VVU/UKIMWI, Dkt. Stephen Ayisi Addo amesema katika ripoti iliyowasilishwa na gazeti la serikali, inaonesha takwimu za maambukizi haya mapya ni kubwa na hivyo kutaka uwepo wa utoaji wa elimu kuhusu ugonjwa huo.
“Takwimu za maambukizi haya mapya ni kubwa mno, hivyo tunatakiwa kuimarisha elimu ili kuwafahamisha watu kwamba VVU bado ni halisi; …Tunapaswa kuwafahamisha watu kwamba wanahitaji kushikamana na mikakati ya kuzuia,” amesema Dkt. Addo.
Aidha amefafanua kuwa, wengi kati ya watu 23,495 waliopimwa ugonjwa huo na kugundulika kuwa na maradhi hayo wamepatiwa matibabu ya VVU ambapo pia ametaja takwimu hizo kuwa ni za kuridhika na ujinga akieleza kwamba uhamasishaji kwa wahudumu wa afya umepungua.
“Baadhi ya vijana leo hawajui kama virusi vya Ukimwi VVU vipo na wengine wanajua vipo lakini wanadhani kwamba vimetoweka, wengi wao wanaogopa zaidi ugonjwa wa Uviko-19 na homa ya Marburg kuliko UKIMWI,” alisema Addo.
Ameongeza kuwa, hadi kufikia Desemba 2021, makadirio ya watu wanaoishi na VVU nchini humo walikuwa watu 350,000, na asilimia 71 pekee ndio waliotambuliwa na mpango huo wa udhibiti ambapo kati ya idadi hiyo, zaidi ya watu 245,000 sawa na asilimia 99 walikuwa kwenye matibabu hadi Juni mwaka huu.
Hata hivyo, Dkt. Addo amebainisha kuwa takribani asilimia 79 ya waliokuwa na ugonjwa huo na walikuwa wakitumia dawa, wamefikia hatua hiyo isiyoweza kugundulika, ambayo haiwezi kusambaza virusi kwa wengine.
Aliongeza kuwa, maambukizi ya ugonjwa huo ni makubwa zaidi kwa wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume, huku kiwango cha maambukizi kikiwa asilimia 18 na kwa wanawake wanaofanya biashara ya ngono wakiwa na maambukizi ya asilimia 4.6.