Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amemtaka mpinzani wake mkuu, Raila Odinga kuchagua kujiengua kwenye uchaguzi wa marudio au kutulia na kuacha kuvuruga utulivu wa nchi hiyo.

Kauli hiyo ya Kenyatta imekuja wakati ambapo Raila na ngome ya NASA wameandaa maandamano kupinga uchaguzi wa marudio wa Oktoba 26 kusimamiwa na Tume ya Uchaguzi ya IEBC ambayo wamedai iliharibu uchaguzi uliopita.

Akizungumza hivi karibuni katika mkutano wa kampeni katika eneo la Mai Mahiu, Nakuru, Kenyatta alisema kuwa kama Raila anadhani bado hajajiandaa vyema na uchaguzi huo ni bora ajiengue kuliko kuratibu maandamano ambayo yanaathiri biashara na mambo mengine ya kijamii.

“Kama Raila hataki uchaguzi au hajajiandaa, anapaswa kutulia. Tunataka kufanya uchaguzi wa amani. Tunataka wakenya waungane. Tunataka jamii tofauti ziishi pamoja kwa amani,” alisema Kenyatta.

Naye Makamu wa Rais, William Ruto aliwataka viongozi wa NASA kutumia njia za kikatiba kuwaondoa maafisa wa IEBC wasiowataka na sio vinginevyo.

Mahakama ya Juu nchini humo ilibatilisha matokeo ya uchaguzi wa urais uliofanyika Agosti 8 mwaka huu baada ya kubaini kuwa haukuwa huru na haki. Matokeo ya uchaguzi huo yaliyotangazwa na IEBC yalimpa Kenyatta ushindi wa asilimia 54. Mahakama hiyo iliamuru uchaguzi mpya kufanyika ndani ya siku 60.

Mwanamke ajioa nchini Italia
Polisi amuua kwa risasi mpenzi wake kisha kujiua