Afisa wa jeshi la polisi eneo la Nakuru nchini Kenya amedaiwa kumuua mpenzi wake kwa kumpiga risasi jana jioni kisha naye kujiua kwa kutumia bunduki aina ya AK 47.

Afisa huyo aliyetajwa kwa jina la Stephen Mungai aliyekuwa akifanya kazi katika kituo cha polisi cha Molo anadaiwa kumpiga risasi tatu mpenzi wake ambaye pia ni mama watoto wake.

Walinzi binafsi wa eneo hilo walisimulia namna ambavyo walisikia ugomvi na kisha milio ya risasi ndani ya nyumba hiyo.

“Nilisikia mwanamme akipigana na mke wake na mwanaume alikuwa akimchapa kwa fimbo. Wakati tunajiandaa kwenda kutoa msaada, tulisikia milio ya risasi,” alisema mlinzi mmoja wa eneo hilo.

Nao majirani walieleza namna walivyowaifahamu familia hiyo ambayo ilihamia katika eneo hilo katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja.

Walisema kuwa usiku huo walimsikia mtoto akilia “baba anamuua mama!” kisha wakasikia milio ya risasi zaidi ya tatu ndani ya nyumba hiyo.

Majirani hao walieleza kuwa mwanamke huyo ndiye aliyekuwa anakaa katika nyumba hiyo na mwanaume alikuwa anamtembelea mara kwa mara.

Mkuu wa jeshi la polisi wa Nakuru, OCPD Joshua Omukatta amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa uchunguzi umeanza kubaini chanzo chake.

Kenyatta amtolea uvivu Raila, amtaka ajiengue au ...!
Chelsea, Man Utd zatamba ugenini michuano ya klabu bingwa